2015-05-07 15:09:00

Msikate tamaa, jipeni moyo na kusonga mbele kwa imani na matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 6 Mei 2015 kabla ya kwenda kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya Katekesi yake, alikutana na kusalimiana na watoto wenye ulemavu kwa kuwashukuru na kuwatia moyo kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa. Hawa ni watoto wanaohudumiwa kwenye vituo vya walemavu kutoka Brindisi.

Watoto hao wamemshukuru Baba Mtakatifu ambaye amewaomba kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala zao. Kwa pamoja walisali, kumwomba Bikira Maria awasaidie katika hija ya maisha yao na baadaye akawapatia baraka zake za kitume. Baba Mtakatifu amesalimiana mmoja mmoja na watoto na wahudumu wao, ambao jumla walikuwa ni watu 30.

Watoto hawa wamemzawadia Baba Mtakatifu michoro mbali mbali walioiandaa kwa moyo mkuu na bashasha. Wahudumu wa watoto hawa wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wataendelea kutekeleza dhamana na utume wao na watoto hawa kwa kujenga na kuimarisha Jumuiya ya upendo na mshikamano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.