2015-05-06 16:24:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Sita ya Kipindi cha Pasaka


Mpendwa msikilizaji wa tafakari ya Neno la Mungu, tunaendendela pamoja kuonja upendo wa Mungu katika kipindi bado cha Pasaka. Leo tunatafakari Dominika ya sita ya Pasaka mwaka B. Mama Kanisa ametuwekea Neno la Mungu litupalo ujumbe maalumu na ndio huu, Mungu atualika kupendana kama yeye alivyotupenda. Ni kwa njia ya upendo Mungu amejidhirisha kwa wanadamu wote. Kumbe basi tukimpenda yeye na kuwapenda wengine tutakuwa watoto wake.

Mpendwa, Ujumbe huu tunaupata katika Somo la Injili ambapo Mwinjili Yohane aliye mwalimu wa upendo anasema akinukuru maneno ya Bwana “kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi kaeni katika pendo langu” Kwa maneno haya ya Kristo tunaalikwa daima kuvaa vazi la upendo kama nguzo ya maisha ya kikristo.Mwinjili Yohane haachi upendo ukielea juu ya maji bila mwelekeo, bali anasema ili kukaa katika pendo la Kristu ni lazima mmoja azishike amri za Mungu ambazo daima ni dira na kielelezo cha mapendo ya Mungu kwa mwanadamu. Kielelezo na mfano kamili usio na doa wa namna ya kushika amri za Mungu ni Kristu mwenyewe ambaye alikaa katika pendo la Baba yake.

Katika kushika amri za Mungu na kupendana kuna pia sadaka kubwa ambayo lazima kuitoa daima, nayo ni kujitoa maisha kwa ajili ya wengine kama Kristu alivyotoa maisha yake kwa ajili yetu sisi. Kristu anazidi kusisitiza kuwa kama mmoja atafanya haya yote atakuwa rafiki yake. Hata hivyo Kristu akijua udhaifu wa mwanadamu ambaye aweza kupata kiburi kuwa ni chaguo lake kumpenda Mungu, anaweka tahadhali akitukumbusha kuwa sio sisi tuliomchagua yeye bali yeye alituchagua sisi. Kumbe yote mema tufanyayo yawe kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Kwa kukazia ujumbe huu somo la pili linatuambia kuwa kupendana sisi kwa sisi ndiyo njia ya kumjua Mungu. Hakuna njia nyingine maana Mungu ni pendo tu! Kwa namna hiyo asiyependa hawezi kusema anamjua Mungu. Hili ni fundisho kubwa mno na latudai tafakari ya hali ya juu kila siku ya maisha yetu. Latudai tafakari maana kadiri ya maisha yetu kuna shida nyingi ambazo zinazuia upendo, zinajenga tabaka la juu na la chini na kwa namna hiyo kwa kukosa upendo tunakosa dira ya kumwelekea Mungu na badala yake tunaweza kuanguka kwa kuwaelekea wafalme wa dunia yaani fedha, madaraka na ubinafsi unaopingana na maisha ya jumuiya na amani.

Mtume Petro katika Somo la kwanza anaposimama na kumwambia Kornelio asimwangukie miguuni, ataka kukwambia wewe unayeshikiria madaraka kama nguzo ya maisha ukaiache na kushika nguzo ya upendo kama Bwana alivyotufundisha. Mtume Petro yuko katika kazi ya umisionari anafundisha na kutangaza ukuu wa Mungu na jinsi alivyotupenda sote bila upendeleo. Anataka kuvunjilia mbali hali ya Wayahudi kujisikia kuwa wao ndio wateule na hivi wengine ni daraja la pili. Anatangaza kuwa Mungu hana upendeleo kwa awaye yote, wote ni watoto wake kwa njia ya Yesu Kristu.

Nasi wapendwa katika jumuiya zetu, kanisani petu na nchini petu wapo watu wanaojisikia wakubwa kuliko wengine, wenye akili kuliko wengine, wenye uchumi imara kuliko wengine, basi mwaliko ni kujisikia familia moja yenye watu wenye vipaji mbalimbali kwa ajili ya utajiri wa familia ya Mungu. Viongozi wajisikie wajibu wa kutumikia zaidi kuliko kutumikiwa, kuwaunganisha wanafamilia na si kuwatenganisha kwa sababu ya dhuluma mbalimbali zinazojikita katika tamaa ya mambo ya kidunia.

Mpendwa, furaha ya pasaka ni wajibu wa upendo, ni wajibu wa kushiriki kujitoa maisha kama Bwana alivyojitoa kwa ajili ya wote. Asante sana, tukutane siku nyingine kama ya leo. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.