2015-05-06 10:20:00

Sakramenti ya ndoa ni kielelezo cha imani na mapendo thabiti!


Ndoa ya Kikristo ina uzuri wake kwani hii ni Sakramenti inayoadhimishwa ndani ya Kanisa pamoja na kusaidia mchakato wa ujenzi wa Jumuiya mpya, Kanisa familia ya Mungu inayowajibika pamoja na jamii. Hili ni fumbo kuu linalonesha uhusiano wa upendo wa dhati kati ya Kristo na Kanisa lake; hiki ni kielelezo makini cha upendo na imani ya Kanisa. Ndoa ni sehemu ya mpango wa kazi ya uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu na kwa njia ya neema na baraka za Mwenyezi Mungu, wakristo wameweza kuishi Sakramenti hii katika utimilifu wake.

Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 6 Mei 2015, kama sehemu ya mwendelezo wa tafakari juu ya maisha ya ndoa na familia, maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Baba Mtakatifu anasema ndoa ni tendo la imani mintarafu mpango wa Mungu kwa binadamu na ni kielelezo cha sadaka ya upendo.

Mtakatifu Paulo katika nyaraka zake anaoanisha upendo wa Kristo kwa Kanisa lake kama ulivyo upendo kwa watu wa ndoa wanavyopaswa kupendana kwa dhati, kama Kristo alivyolipenda Kanisa kiasi cha kujisadaka kwa ajili yake. Pale ambapo mwanaume na mwanamke wanaamua kuoana katika Kristo Bwana, wanashiriki katika umissionari wa Kanisa, kwa kuishi si tu kwa ajili ya familia zao, bali kwa ajili ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kutokana na ukweli huu, maisha na utume wa Kanisa yanarutubishwa na kila ndoa inayofungwa Kanisani, kwani zinaonesha ule uzuri wa ndoa; Kanisa linadhalilishwa pale ndoa inapobomolewa. Wanandoa wanaoishi kikamilifu na kwa ujasiri neema ya Sakramenti ya Ndoa, wanalisaidia Kanisa kutoa zawadi ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wote sanjari na kuwasaidia watu wengine kuonja zawadi hizi katika maisha ya ndoa na familia zao. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna waamini ambao kweli wanajitahidi kuliishi Fumbo hili kwa ukamilifu wake, kwa kujiaminisha kwa Mungu na tunza kutoka kwa Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko akisalimiana na mahujaji katika lugha mbali mbali anawakumbusha kupyaisha upendo wao kwa Bikira Maria, mwanzoni mwa Mwezi Mei, uliotengwa na Kanisa kwa heshima ya Bikira Maria, kwa kutenga muda wa kukaa, kukatafakari na kusali na Bikira Maria. Waendelee kumwomba Yesu Kristo ili aweze kuimarisha imani yao na familia zao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuendelea kuwasindikiza wanandoa wapya kwa njia ya sala na sadaka zao, ili waweze kuishi kikamilifu neema ya Sakramenti ya Ndoa, kwa kushuhudia uzuri na utakatifu wa Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Wakumbuke kwamba, daima Yesu Kristo Mfufuka yuko pamoja nao katika hija na medani mbali mbali za maisha; wakati waraha na karaha; wakati furaha chereko, ili kushuhudia umuhimu wa upendo wa Mungu unaojikita katika uaminifu katika Sakramenti ya Ndoa, Fumbo kuu katika maisha na utume wa Kanisa kama anavyosema Mtakatifu Paulo.

Hija za kiroho zinazofanywa na waamini ziwasaidie kukuza hamu ya kulitafakari Neno la Mungu, ili waweze kuwa ni watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu na mashuhuda wa ujenzi wa utamaduni wa upendo. Bikira Maria Mama wa Mungu awe ni kimbilio kwa wanandoa wapya na wagonjwa ili aweze kuwasaidia kupita katika magumu ya maisha na kujenga familia zao ili ziweze kuwa ni shule ya sala na maelewano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.