2015-05-06 16:09:00

Leo wote kidole juu, yaani we acha tu! Ni raha kwenda mbele!


Asiye na mwana eti aeleke jiwe! “Mpeeeniii rahaaaa … mpeni raha ... aaeeeh” haya ni maneno ya wimbo wa kumshangilia kiongozi au mtu mwenye kusherehekewa sikukuu fulani. Mashabiki wanamwimbia mtu wanayempenda na kumtakia raha na furaha. Kila binadamu anapenda raha na kuishi kwa furaha, lakini huwezi kufurahi au kuwa na raha kama hakuna upendo. Mtoto mchanga anafurahi anapoonja upendo wa mama yake. Kwa hiyo lengo la kupenda ni kuwa na furaha, na furaha ya mtoto ni alama kuwa upendo wa mama upo ndani yake, na ameungana sana mama yake. Furaha ni kiwango na kipimo kinachoonesha kuwa unaishi vizuri na mambo yako yamekunyokea. Hapo hata usipoimbiwa “mpeni raha,” basi mwenyewe utajipa raha na kufurahi.

Jumapili iliyopita tulitafakari juu ya mti wa Mzabibu wenye kazi moja tu ya kuzaa. Mzabibu usiozaa haufai kwa jambo lingine lolote lile. Mmea wa Mzabibu unatoa uhai (utomvu) kwa matawi ili yaweze kuzaa zabibu na kutengeneza divai ichangamshayo na kuleta raha au furaha. Wayahudi walijilinganisha na mzabibu ulioungana daima na Mungu na kutoa matunda, lakini kinyume chake matendo yao yalikuwa chukizo kwa Mungu na yaliwaletea watu karaha badala ya raha na furaha.

Yesu alijitangaza mwenyewe kuwa ni mzabibu wa kweli na Baba yake ndiye mkulima. Leo Yesu anatuonesha kwamba ameungana kabisa na Baba yake, na anatutakia sisi kuungana naye katika upendo. “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi.” Upendo siyo kitu kilichotengenezwa au kuundwa na binadamu, la hasha, bali ni uhalisia ulioko katika uumbaji. Upendo ni kama nyumba ya kuishi, au kama kijiji au nchi ya kukaa. Kwa hiyo Yesu anatualika “Kaeni katika pendo langu.” Sanasana tuko tayari ndani ya upendo yaani tunaishi katika upendo kama mtoto ndani ya tumbo la mama.

Unakaa ndani ya pendo la Kristu kwa hiari. Yesu hakulazimishi kulikubali pendo lake, bali anakutakia utambue kuwa uko ndani ya pendo la Mungu na udumu kujilinganishe na roho hiyo. “Mkishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu.” Yesu mwenyewe alikubali kufanana na Mungu, yaani alikubali kuwa damu ya kundi moja na Mungu. Kadhalika wanaomfuata Yesu wanakuwa naye damu kundi moja. Wanachoweza kufanya ni kutumia uhuru wao kuchagua kubaki ndani ya pendo hilo au la.  Yesu hakuwa anapenda ili apate mshahara au nishani ya upendo toka kwa Mungu, bali alivutwa tu na huluka ya kupenda bila kutegemea malipo. Kadhalika Mkristo asifanye matendo ya upendo kwa ajili ya kulipwa mshahara au kupata thawabu au nishani fulani toka kwa Mungu, kwani mfuasi wa Kristo anaongozwa na roho ya Kristo.

Binadamu tumezaliwa na huluka ya kupenda lakini hatuwezi kutosheka na upendo hadi tumempenda. Kwa hiyo nishani na mshahara wa upendo wa kweli ni kuwa na furaha ya kweli na inayodumu. Ndiyo maana Yesu anasema: “Hayo nimewambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu na furaha yenu itimizwe.” Sisi tunakuwa na furaha endapoa tunakuwa sisi wenyewe. Tunakuwa sisi wenyewe kwa vile tu watoto wa Mungu kwa sababu tupo damu kundi moja naye. Furaha hiyo ndiyo alama wazi ya ufunuo wa Mungu ndani yetu. “Mkijua mambo haya mtakuwa wenye heri hasa mkilitimiza.” Kuwa na raha au furaha ndiyo heri kuu aliyotuahidia Yesu.

Yesu anatoa mwongozo wa kupenda anaposema, “Pendaneni ninyi kwa ninyi.” Yaani kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na kile tunachokipenda, na siyo kupenda utu au ubinadamu ambao hauonekani, bali unampenda mtu huyu, mtoto yule au fukara huyu. Kadhalika upendo huu nao hautoshi kwani watu wengi wanapendana tena kwa namna mbalimbali, kumbe yabidi upendo utoke kwa Kristu mwenyewe kama anavyosema, “Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi,” yaani kupenda kadiri ya Mungu kwa sababu kipimo pekee cha upendo ni kumpenda Mungu bila kipimo.

Mkristo anapenda kama Kristu, na kwa jinsi alivyopenda Yesu, kwa sababu upendo huo wa Kristo unatiririka kama damu toka kwa Mungu mwenyewe ukipitia kwa Kristu hadi kutufikia sisi na hatimaye kumwendea kila mtu. Kwa hiyo yabidi kila mmoja azibue mishipa inayomwunganisha na Mungu ili kupitisha upendo wake. Yabidi kuzibua mifereji ili maji yamwagilie ulimwengu ulio mkavu kwa upendo. Ukiuziba mshipa wa upendo ndani yako hapo furaha inakufa.

Marafiki wanapendana na wanasaidiana katika dhiki, na mapato yake wanafurahiana na kupeana raha. “Ninyi ni rafiki zangu mkitenda niwaamuruyo.” Rafiki wa kweli anakuwa nawe uwapo katika dhiki, kadhalika marafiki wa kweli hupeana zawadi bila kulipana au kukadiria malipo. Hivi ndivyo anavyotuita Kristu kuwa tu rafiki zake. Aidha, Yesu anaukaribia zaidi utu wetu wa kibinadamu anaposema “Siwaiti tena watumwa; lakini ninyi nimewaita rafiki:” Kuwa rafiki wa Mungu maana yake ni kuwa sawa na Mungu. Yeye aliye mfalme na Bwana mkuu, anakuwa rafiki. Upendo aina hii unatuletea zawadi nyingine zaidi ya furaha, nayo ni hekima pale anaposema: “kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewataarifu.” Kwa njia ya upendo, mmoja unakuwa na furaha na kumfahamu Baba yaani unakuwa na hekima ya kuishi, ya kujifahamu na kuufahamu ubinadamu.Yesu aliyekuwa fukara wa kila kitu, huyo kumbe ni tajiri mwenye marafiki wengi, anasherekea kwa furaha uzuri wa urafiki huo na anatudokezea jina jipya la Mungu nalo ni Rafiki. Mungu ni rafiki yetu kwa vile anatupa raha na furaha. “Mpeni raha Kristo mpeni raha, aaeeeh!”

 

Na Padre Alcuin Nyirenda. OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.