2015-05-05 11:27:00

Jikiteni katika imani, matumaini na mapendo ili kukabiliana na magumu!


Mkristo ni mwamini anayepambana na matatizo pamoja na changamoto za maisha kwa imani na matumaini pasi ya kukata tamaa; ni mtu anayejiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu akitumainia ulinzi na tunza yake na kwamba, amani na usalama kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni silaha madhubuti ya kusonga mbele katika maisha na utume wa Kanisa kama walivyofanya Mitume wa Yesu.

Mtakatifu Paulo aliteswa, lakini akasimama imara na thabiti katika imani, kiasi cha kuwaimarisha ndugu zake kuendelea kumtumainia Mungu. Neno la Mungu linasema kwamba, imewapasa kukabiliana na mateso na magumu katika maisha kabla ya kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumanne, tarehe 5 Mei 2015 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, Mkristo anapaswa kubeba mateso na mahangaiko kwa ujasiri na moyo mkuu, kama ilivyo pia katika hija ya maisha ya kila siku, pamoja na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ambaye ana uwezo wa kuwakirimia waja wake nguvu na uwezo wa kudumu katika imani na matumaini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiaminisha kwa Kristo na kuwaaminisha ndugu zao kwa Kristo kwani hii ni sala ya Kikristo inayobubujika kutoka katika moyo wenye matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Yesu alipokuwa anawaaga wanafunzi wake, alipenda kuwaachia amani inayojikita katika undani wa mtu, kiasi cha kumkirimia nguvu inayodumisha imani, matumaini na mapendo. Mateso na mahangaiko ni sehemu ya hija ya maisha ya mwanadamu, lakini waamini wanapaswa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu ambaye kamwe hawezi kuwadanganya. Waamini wajitahidi kumwomba, Yesu Kristo ili wakirimie fadhila ya imani, matumaini na mapendo, ili kushinda magumu ya maisha, kwani Yesu ni kielelezo cha ushindi huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.