2015-05-05 14:47:00

Dumisheni umoja, udugu, mshikamano na maridhiano, ili kujenga amani!


Viongozi wa kidini nchini Ufaransa wanasikitishwa sana na hali inayoendelea kujitokeza nchini humo kutokana na ukosefu wa amani, utulivu na maridhiano yanayofanywa kwa misingi ya imani kali za kidini. Viongozi hawa wanakumbusha kwamba, wote ni watoto wa Mungu na tofauti zao za kidini zisiwe ni sababu ya chokochoko na vurugu, bali amana kubwa inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wengi.

Viongozi wa kidini katika tamko lao la pamoja, wanalaani vikali uvunjifu wa misingi ya haki na amani inayofanywa na baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kidini, inayopelekea hofu na wasi wasi kwa wananchi wengi nchini Ufaransa. Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na kunajisiwa kwa makaburi, nyumba za ibada na makazi ya watu kwa kisingizio cha imani kali. Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali nchini Ufaransa na wapenda amani kusimama kidete kulaani na kupinga vitendo hivi vya uvunjifu wa misingi ya amani, utulivu na maridhiano kati ya watu.

Tabia ya kulipizana kisasi ni jambo ambalo limepitwa na wakati na wala si sehemu ya suluhu ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Watu wajifunze kujenga utamaduni wa haki, msamaha, upatanisho na maridhiano kwa ajili ya mafao ya wengi. Hakuna sababu ya kutishiana maisha na kuendekeza kinzani na misigano isiyokuwa na mafao kwa watu. Nyumba za ibada zinapaswa kuwa ni mahali pa sala, upendo, umoja na mshikamano. Tofauti za maisha ya kiroho ni utajiri mkubwa kwa wananchi wa Ufaransa katika ujumla wao.

Katika siku za hivi karibuni chokochoko dhidi ya Wakristo, Wayahudi na Waislam zinaendelea kuongezeka kwa kasi ya ajabu nchini Ufaransa. Umefika wakati wa kujenga na kuimarisha utamaduni wa mshikamano, maridhiano na majadiliano ya kidini, kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Watu wachache wasipewe nafasi ya kuvuruga amani, utilivu na maridhiano kati ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.