2015-05-04 14:48:00

Wakristo simameni kidete kutetea utu, heshima na tunu msingi za ndoa!


Mama Kanisa hivi karibuni ameadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka juu ya Majadiliano ya Kiekumene, Unitatis Redintegratio, dira na mwongozo katika mchakato wa kiekumene kati ya Wakristo. Huu ni mwaliko kwa Wakatoliki kusoma alama za nyakati na kufanya maamuzi ili kujikita katika hija ya umoja na hivyo kuondokana na migawanyiko kati ya Wakristo, jambo linalokwenda kinyume cha utashi wa Kristo na kashfa katika utangazaji wa Habari Njema kwa kila kiumbe.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanatambua na kuthamini mchango wa Wakristo wa Makanisa na madhehebu mbali mbali ya Kikristo kuwa ni ndugu katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Wakatoliki na Waluteri wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba, wanashikamana ili kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo katika ngazi mbali mbali. Lengo ni kuweza kuwa na alama wazi za umoja katika: Imani, Sakramenti, Huduma za Kikuhani; mambo ambayo bado yanapaswa kufanyiwa kazi kubwa, ili kuweza kufikia umoja kamili miongoni mwa Wakristo.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 4 Mei 2015 alipokutana na kuzungumza na Dr. Antje Jacklèn, Askofu mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri la Uppsala, nchini Uswiss. Baba Mtakatifu ana matumaini makubwa kwamba, hati ya pamoja kati ya Waluteri na Wakatoliki inayowahamasisha kutoka katika kinzani na kuanza mchakato wa umoja na mshikamano kuelekea maadhimisho ya pamoja hapo mwaka 2017 ni muhimu sana, katika mchakato wa umoja wa Wakristo.

Huu ni mwaliko pia wa kuendelea kushikamana katika huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa njia ya ushuhuda makini unaotolewa na Wakristo wote. Ni changamoto kwa wakristo wote kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, tunu msingi za maisha ya ndoa na familiapamoja na tofauti za kijinsia katika kukamilishana.

Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Uswiss kwa kuwapokea na kuwarimia wakimbizi na wahamiaji kutoka Amerika ya Kusini. Amemshukuru kwa kumkumbusha rafiki yake mchungaji Anders Root ambaye wameshirikishana mwengi katika tafakari za kitaalimungu kwa maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.