2015-05-04 15:47:00

Uhaba wa madawati Tanzania ni tatizo la kitaifa, wananchi changieni!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameahidi kuchangia madawati 135 na viti vyake kwenye Shule ya msingi Kiembesamaki iliyoko wilaya ya Magharibi mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni mwitikio wa maombi aliyopewa na shule hiyo. Ametoa ahadi hiyo Jumamosi, Mei 2, 2015, wakati akikabidhi msaada wa madawati 45 na viti vyake yenye thamani ya sh. milioni 3.83/- yaliyotolewa na kampuni ya Jambo Plastics ya Dar es Salaam ili kupunguza uhaba wa madawati katika shule za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

“Tatizo la madawati ni la kitaifa… Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali ametuambia kwamba haya ya leo yatatosha darasa moja tu na bado kuna mengine matatu hayana kabisa madawati. Changamoto iliyopo hivi sasa ni kwamba haya madawati yatagawanywa vipi wakati watoto wengine bado hawana mahali pa kukaa?” alihoji Waziri Mkuu.

“Ili kuondoa tatizo hilo, mimi nitachangia madawati yaliyobakia kwa madarasa hayo matatu ili watoto wetu wakae vizuri, wazingatie masomo yao na pia wawe na miandiko mizuri,” alisema huku akishangiliwa na walimu, wanafunzi na baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo waliohudhuria hafla hiyo. Madawati hayo 135 na viti vyake vina thamani ya sh. milioni 11.5 kwa bei ya sh. 85,000/- kwa kila dawati na kiti chake.

Alipoulizwa ni lini madawati hayo yatakuwa tayari, Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bibi Rupa Suchak alisema yatawasilishwa shuleni hapo baada ya wiki moja kwa sababu wana madawati ambayo yamekwishatengenezwa kwenye bohari za kiwanda chao.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuongea na jumuiya iliyofika kushuhudia utolewaji wa msaada huo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Bw. Ali Juma Shamhuna alisema yeye alisoma kwenye shule hiyo mwaka 1952 na kuainisha kwamba wana uhaba wa madawati kwa madarasa manne.

“Tunayo madarasa matupu manne na hii ndiyo skuli yangu niliyosoma tangu mwaka 1952. Ni kweli tunakua na tunaongezeka lakini bado tuna watoto wanakaa chini… wananchi wa Zanzibar wanajitolea kujenga shule lakini inapofika kwenye madawati imekuwa ni tatizo. Tunaomba kuungwa mkono zaidi”, alisema.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi, Bw. Ayoub Mahmoud Jecha alisema shule hiyo ina shule za Serikali 64 lakini ni shule mbili tu ndizo zina madarasa yaliyokamilika na yote yakiwa na madawati. Alisema wilaya hiyo ina jumla ya wanafunzi 114,000 ambapo 79,000 kati yao wanasoma kwenye shule za Serikali na 35,000 wanasoma kwenye shule za binafsi.

“Wilaya hii ina upungufu wa madawati 5,700. Kwa uwiano wa dawati moja kwa kila watoto watatu, ina maana kuwa watoto 17,100 wanasoma wakiwa wamekaa chini. Tunashukuru mchango huu wa Jambo Plastics lakini tunaomba wahisani zaidi wa kutusadia ili watoto wetu wapate mazingira mazuri ya kujifunzia,” aliongeza.

Awali, Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jambo Plastics, Bibi Rupa Suchak katika taarifa yake alisema kampuni yake imeamua kutumia plastiki kutengeneza madawati kwa sababu imedhamiria kuhifadhi mazingira lakini kuokoa kudorora kwa uchumi.

“Haya madawati ni imara na yanadumu kwa muda mrefu tumeshayasambaza kwenye shule zaidi ya 400 huko Tanzania Bara na tumeona matokeo mazuri… pia yanasaidia kuhifadhi mazingira kwa kuzuia ukataji miti ovyo. Takwimu zinaonyesha miti zaidi ya 100,000 inakatwa kila mwaka kwa ajili ya kupata mbao za kuetengezea madawati,” alisema.“Madawati haya yanaweza kuongezwa au kupunguzwa urefu kulingana kimo cha mtoto lakini pia yana uimara wa pekee ambao unaokoa mamilioni ya fedha ambazo zingetumika kununua madawati mengine pindi yale ya mbao yanapovunjika,” alisema.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.