2015-05-02 16:36:00

Jimbo kuu la Cotonou Benin: Sinodi ya kwanza ya Jimbo: Vipaumbele


Imani na mafundisho tanzu ya Kanisa yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; sera na mikakati bora ya kijamii, kiuchumi na kielimu; ni kati ya mambo yaliyopembuliwa na Familia ya Mungu Jimbo kuu la Cotonou, Benin katika maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo iliyohitimishwa hivi karibuni. Ibada ya Misa ya shukrani imeongozwa na Askofu mkuu Antoine Ganyè wa Jimbo kuu la Cotonou na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo hilo.

Baada ya maadhimisho, washiriki wa Sinodi ya Jimbo wamemkabidhi mapendekezo ya Mababa wa Sinodi, yatakayopitiwa na Askofu mahalia, ili hatimaye, yaweze kufanyiwa kazi katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Cotonou, Benin. Lengo ni kuyatakatifuza malimwengu, kwani wao ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Familia ya Mungu inapaswa kuonesha mshikamano na Kanisa zima katika mambo msingi ya maisha na utume wake. Hii ndiyo changamoto ambayo Jimbo kuu la Cotonou linataka kuifanyia kazi mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo.

Askofu mkuu Antoine Ganyè anabainisha kwamba, Wakristo washikamane na kufanya kazi katika umoja, upendo na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na jamii inayowazunguka. Waongozwe na kanuni ya upendo na udugu inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Na kwa njia ya Sakramenti hii, waamini wote wanashiriki katika: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo. Na kwa njia hii, Jimbo kuu la Cotonou, Benin linajiandaa pia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayoanza kutimua vumbi mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi 25 Oktoba 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.