2015-05-02 10:41:00

Iweni watu wa matumaini, mshikamano, ari na mwamko mpya wa kimissionari


Familia ya Mungu kutoka Jimbo Katoliki la Isernia-Venafro, Jumamosi tarehe 2 Mei 2015 wamemtembelea Baba Mtakatifu Francisko kumshukuru kwa hija ya kitume aliyoifanya Jimboni mwao, tarehe 5 Julai 2014. Baba Mtakatifu amewashukuru wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma ya Injili na kuwataka kusimama kidete ili kukabiliana na matatizo makubwa na changamoto wanazokabiliana nazo. Changamoto hizi ni: ukosefu wa fursa za ajira; huduma hafifu kwa wazee, wagonjwa, walemavu na familia. Huu ni mwaliko wa kuunganisha nguvu za pamoja kati ya Serikali na wadau mbali mbali ili kupata fursa za ajira kwa vijana ili waweze kufanya kazi halali na kujipatia riziki yao yak ila siku.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwahimiza Watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Isernia-Venafro kuwa na ari na mwamko wa kimissionari, ili kuweza kufaidi matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Celestino inayoendelea Jimboni humo. Huu ni mwaliko wa kumrudia Kristo, Injili na kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, ili kuweza kuwamegea wengine upendo wa Mungu. Hawa ni wale watu pweke, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu ambao hawatedewi haki na jamii; watu ambao wamechoshwa na maneno matupu na sasa wanasikia ndani mwao, ile hamu ya kuwa na Mungu.

Baba Mtakatifu anawahimiza waamini wa Jimbo Katoliki la Isernia-Venafro kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha vyema zaidi Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Iwe ni fursa ya kuwa na ari na mwamko mpya wa shughuli za kimissionari Parokiani na katika vyama vya kitume, kama kielelezo cha umoja wa Kikanisa. Kila Jumuiya iwe ni mahali muafaka pa kusikiliza Neno la Mungu; nyumba zao ziwe ni mahali pa sala pamoja na kushiriki katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa kuonesha uchaji na moyo wa Ibada.

Waamini wajitahidi kuwa na matumaini ya Kikristo katika shida na mahangaiko yao; wawe ni vyombo vya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kujenga na kuimarisha jamii inayojikita katika ukarimu, heshima, haki na mshikamano. Changamoto hizi wanaweza kuzikabili kwa kuonja uwepo endelevu wa Yesu katika maisha yao, hususan kwa vijana kusaidiana, ili kuvuka vikwazo na changamoto za maisha kwa njia ya mshikamano, unaopaswa kushuhudiwa katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anawaweka waamini wa Jimbo Katoliki la Isernia-Venafro chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia kuwa wanyenyekevu, ili hatimaye, wawe mitume: wanyenyekevu, waaminifu na makini kwa Injili ya Kristo. Bikira Maria pamoja na watakatifu wote waliowaombea katika hija ya imani yao, wawasaidie kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.