2015-05-02 10:29:00

Fra Junìpero: Mmissionari mahiri, mwenye Ibada na Shuhuda wa utakatifu


Mama Kanisa anatumwa na Yesu kwenda ulimwenguni kote ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu, dhamana hii imetekelezwa na Wakristo wa Kanisa la mwanzo, tangu wakati ule walipoanza kudhulumiwa na kuendelezwa na Wamissionari wa nyakati mbali mbali hadi kufikia kwa Fra Junìpero Serra, aliyesimama kidete kutetea utu wa mwanadamu pamoja na kuinjilisha. Akawa ni kati ya “Mitume 12 wa Shirika la Wafranciskani” waliotumwa kuinjilisha nchini Mexico.

Haya yakawa ni mapambazuko mapya ya Uinjilishaji ambao tayari ulikuwa umekwisha tekelezwa na wamissionari kutoka Hispania, Florida na Califonia. Fra Junìpero akajipambanua kwa mambo makuu matatu: ari na moyo wa kimissionari; Ibada kwa Bikira Maria na Ushuhuda wa Utakatifu wa maisha. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 2 Mei 2015 wakati alipotembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Wamarekani, kilichoko mjini Roma

Fra Junìpero aliacha yote na kuamua kuzama katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu, ili kuwashirikisha wengine, ile furaha ya kukutana na Yesu Kristo, chemchemi ya ukamilifu wa ukweli na wema. Kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, Fra Junìpero alikuwa ni mtu mwenye furaha, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, kwa njia ya maisha na utume wake, watu wengi wamelitambua Fumbo la Utatu Mtakatifu; tayari kujisadaka kwa njia ya ushuhuda wa upendo, changamoto endelevu hata kwa Wakristo wa nyakati hizi anasema Baba Mtakatifu.

Wakati mwingine watu wanajikuta wakizama zaidi katika makando kando na mapungufu yao ya kibinadamu, lakini wanashindwa kutambua ukarimu na ujasiri waliokuwa nao katika kuitikia wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuacha yote ili: kumfuasa, kumwabudu na kumwona katika nyuso za maskini, tayari kuwaonjesha huruma ya Kristo. Ushuhuda wa Fra Junìpero ulimgusa, kiasi cha kujiachilia ili kuwatangazia watu Injili ya Furaha.

Baba Mtakatifu anasema, Fra Junìpero alidhaminisha kazi yake ya kimissionari kwa Bikira Maria, Mama Yetu wa Guadalupe; kwa kuomba neema na baraka ya toba kwa wakoloni na wazawa; akamwongoza nyakati alipokuwa anahubiri na kuanzisha utume huko Califonia, ndiyo maana Mama Yetu wa Guadalupe ni msimamizi wa Bara la Amerika. Ni Mama ambaye alikuwa mtume na mmissionari, akawa ni chemchemi ya faraja na matumaini, tayari kusikiliza kwa makini ili kuwatunza watoto wake kutoka Amerika.

Fra Junìpero alikuwa ni shuhuda wa utakatifu wa maisha, muasisi wa nchi ya Marekani, msimamizi na mlinzi wa Wahispania, ili kwa pamoja Wamarekani waweze kutambua utu wao, ili kuimarisha mshikamano wao na Kristo pamoja na Kanisa lake. Fra Junìpero aendelee kuwa ni mwombezi kati ya watakatifu wengi wanaojipambanua kwa karama na utume wao katika maisha ya Kanisa. Hawa ni watakatifu waliojikita katika maisha ya tafakuri, wachungaji wema; wafanyakazi katika shamba la Bwana; wahudumu wa wagonjwa na maskini; wamissionari mahiri na wafia dini kama Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero.

Baba Mtakatifu Francisko ana matumaini makubwa katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya huruma ya Mungu kwa Familia ya Mungu Amerika. Waendelee kuwa na imani lwa maneno ya Yesu. Waendelee kumwomba Yesu Kristo Mfufuka kukita uwepo wake katika maisha ya Familia ya Mungu Barani Amerika ili kujenga na kudumisha utamaduni wa maisha, udugu, mshikamano, haki na amani; daima kwa kutoa upendeleo wa kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Asaidie kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili ufalme wake uweze kuenea duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.