2015-05-01 07:20:00

Siku Kuu ya Wafanyakazi: Ukosefu wa fursa za ajira, matumaini na haki


Mei Mosi, kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, siku ambayo wafanyakazi wanaitumia kwa ajili ya kutafakari na kutathmini masuala ya kazi zilizofanyika, tayari kujiwekea mikakati ya kuboresha utendaji wa kazi na ushirikishwaji wa wadau mbali mbali katika sekta ya kazi. Ni siku ya kuonesha mshikamano kati ya wafanyakazi na waajiri wao; kati ya wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi: muda wa kuangalia sheria, haki na wajibu katika masuala ya: uzalishaji na utoaji wa huduma.

Wachunguzi wa masuala ya kiuchumi wanabainisha kwamba, kunaweza kuwepo kwa ongezeko la mishahara, hali nzuri na mazingira bora ya kazi, ikiwa kama tija, uzalishaji pamoja na ufanisi kazini vitazingatiwa. Mchango wa wafanyakazi usaidie kukuza pato la wafanyakazi. Lakini ubadhirifu wa mali ya umma, ufisadi, wizi na hujuma ni mambo yanayoweza kukwamisha juhudi na mafanikio katika uzalishaji, ugavi na utoaji wa huduma. Kumbe sheria za kazi, utawala bora, usalama kazini ni kati ya mambo msingi katika kukuza na kuongeza tija sehemu mbali mbali za kazi.

Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi iliwekwa kunako mwaka 1955 na Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili. Lengo ni kutambua heshima ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kama sehemu ya mchakato wa utimilifu wa utu wa mwanadamu. Ushiriki wa mwanadamu katika kazi ni kuendeleza kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu, ili kuutiisha ulimwengu uwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa ajili ya huduma bora kwa maisha ya mwanadamu.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, Italia, katika mkesha wa maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi duniani kwa mwaka 2015 anapenda kutafakari kwa namna ya pekee mambo makuu matatu: ukosefu wa fursa za ajira, matumaini na haki. Maadhimisho haya yanafanyika wakati Familia ya Mungu Jimboni humo inaendelea kujiaandaa kwa ajili ya ziara ya Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco pamoja na kutembelea Sanda Takatifu, ili kutoa heshima yake.

Itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Torino. Mwaliko ni kuendelea kujenga na kudumisha udugu na mshikamano unaowajibisha. Baba Mtakatifu daima anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee vijana ambao hawana tena matumaini katika maisha kwa kukosa fursa za ajira; kwa familia ambazo zinashindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa vile hazina kazi tena na kwamba zinaendelea kuathirika kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa.

Katika shida na mahangaiko yote haya, kuna haja kwa Mama Kanisa kuendelea kuwajengea waamini imani na matumaini, ili kulinda utu na heshima yao. Ukosefu wa fursa za ajira ni kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Mama Kanisa katika shida na mahangaiko ya binadamu, katika mikakati na sera za uchumi na maendeleo anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kwani binadamu ni rasilimali na nguvu kazi inayopaswa kutumia vyema. Hapa Kanisa litaendelea kupaaza kilio chake kwa wanasiasa na watunga sera kuhakikisha kwamba, mwanadamu anapewa kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya uchumi na maendeleo na kamwe, fedha isiwe ni kipimo cha maendeleo ya watu.

Ikumbukwe kwamba, kazi ni dhamana na wajibu wa kila binadamu; mahali ambapo hakuna fursa za ajira, hapo utu na heshima ya binadamu viko hatarini, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa na kitaifa kujikita katika kutafuta mafao ya wengi sanjari na kuibua mikakati ya uchumi shirikishi, usiobagua wala kudhalilisha watu. Onesho la Sanda takatifu ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya binadamu wa nyakati mbali mbali anasema Askofu mkuu  Cesare Nosiglia. Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka katika wafu, bado anaendelea kufanya hija na watu wake, kwa kuwajengea imani na matumaini katika maisha.

Matumaini ni chachu inayofumbatwa katika maisha ya sala inayomwilishwa katika haki na upendo. Hii ni changamoto kwa taasisi za Serikali na watu binafsi kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa kuwajengea watu matumaini ya maisha bora zaidi, kuliko hali ilivyo kwa wakati huu. Wananchi wanapaswa kuwa na matumaini kwa ajili ya maisha yao na yale ya watoto na watu wanaowategemea. Mji wa Torino kwa miaka mingi umekuwa ni maarufu sana kutokana na ukweli kwamba, huu ni mji wa kiwanda cha magari, maendeleo ya teknolojia; lakini mi mji ambao sasa unashuhudia pengo kati ya maskini na matajiri; kinzani kati ya raia na wahamiaji; changamoto ya kujenga na kuimarisha mshikamano wa umoja, upendo na udugu; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.