2015-05-01 08:23:00

Majandokasisi 14 kutoka Urbaniana kupewa Daraja la Ushemasi wa mpito


Huduma ya Kanisa iliyowekwa na Mwenyezi Mungu hutimizwa kwa njia ya daraja mbali mbali na wale ambao tangu zamani waliitwa: Maaskofu, Mapadre na Mashemasi. Kanisa linafundisha kwamba, kuna ngazi kuu mbili za kushiriki katika huduma ya Ukuhani wa Kristo: Uaskofu na Upadre. Ushemasi umewekwa ili kuwasaidia na kuwahudumia Maaskofu na Mapadre. Kutokana na mafundisho haya, Ushemasi ni ngazi ya huduma. Neema ya Sakramenti ya daraja huwapa Mashemasi nguvu ya lazima kutumikia Taifa la Mungu katika huduma ya: Liturujia, Neno la Mungu na huduma ya mapendo katika umoja na Maaskofu pamoja na Mapadre.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la uinjilishaji wa Watu, hapo tarehe 2 Mei 2015 anatarajiwa kutoa Daraja la Ushemasi wa mpito kwa Majandokasisi 14 kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko hapa mjini Roma. Kuna Majandokasisi 4 kutoka Barani Asia, 10 kutoka Barani Afrika na kati yao kuna Mashemasi 4 kutoka katika nchi za AMECEA nao ni: Frt. Kibirige John Mary kutoka Uganda; Frt. Lyevuze Ssekyanzi Emmanuel kutoka Uganda na Frt. Celestin Zacharia Mauherege kutoka Jimbo Katoliki la Kigoma, Tanzania.

Frt. Celestin Zacharia Mahurege alizaliwa Jimboni Kigoma kunako tarehe 16 Aprili 1980. Baada ya masomo yake ya elimu ya msingi, akajiunga na Seminari Ndogo ya Ujiji, Jimbo Katoliki Kigoma. Baadaye kwa masomo ya kidato cha tano na sita, alipelekwa Seminari Ndogo ya Nyegezi, Jimbo kuu la Mwanza. Alijipatia masomo ya Falsafa kutoka Seminari kuu ya Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba na Taalimungu, alianzia Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma, ambako amejipatia shahada ya kwanza katika taalimungu na sasa, anaendelea na shahada ya uzamili maadili. 

Majandokasisi kwa ujumla wao, wamechagua kauli mbiu inayoongozwa na maneno ”Nanyi mtakuwa mashahidi wangu hadi ukamilifu wa dahari”. Mashemasi watarajiwa wanawaomba muwasindikize katika kipindi hiki cha mpito kwa sala na sadaka zenu, ili kweli waweze kuwa ni majembe ya nguvu katika huduma Altareni, Neno la Mungu na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani ushemasi ni daraja la huduma kwa Familia ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.