2015-04-30 15:54:00

Vatican kusaidia huduma kwa waathirika wa Virusi vya Ukimwi Shinyanga


Mfuko wa Msamaria mwema ambao unasimamiwa na kuratibiwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, PCOS, kwa kushirikiana na Shirika la Famasia la Gilead wamewekeana sahihi mkataba wa kutoa dawa za kurefusha kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, Jimbo Katoliki la Shinyanga, Tanzania. Mkataba huu umewekwa sahihi na Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu kwa niaba ya Baraza la Kipapa na Bwana Gregg Alton, Makamu wa Rais wa Shirika la Famasia na Sayansi la Gilead

Huduma ya dawa za kurefusha maisha anasema Monsinyo Mupendawatu itatolewa kwenye Kijiji cha Bugisi, Jimbo Katoliki Shinyanga, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji kwa vitendo mradi wa miaka mitano wa kupima na kutibu, ulioanzishwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, PCOS chini ya Mfuko wa Msamaria mwema, ulioanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2004 pamoja na Shirika la Famasia na Sayansi la Gilead, lenye makao yake makuu, Califonia, nchini Marekani.

Mradi huu utatoa huduma ya kupima virusi vya ukimwi na wale watakaogundulika kwamba, wameambukizwa na Ukimwi, wataanza kupewa dawa za kurefusha maisha. Mradi huu kwa mara ya kwanza ulizinduliwa Dar es Salaam, Tanzania kunako tarehe 11 Februari 2014. Vituo vitakavyofaidika na mradi huu ni pamoja na: Kituo cha Afya cha Ngokolo, Zahanati ya Buangija na Mija. Kwa njia huu wananchi wanaoishi katika Jimbo Katoliki la Shinyanga na Majimbo jirani wanaweza kupata huduma ya kupima na kupatiwa tiba ya dawa za kurefusha maisha.

Utafiti na uchunguzi uliofanywa hapo awali unabainisha kwamba, kuna zaidi ya watu elfu ishirini ambao wameathirika kutokana na ugonjwa wa Ukimwi Jimboni Shinyanga. Wagonjwa hawa watapatiwa tiba, mara tu mradi huu utakapoanza kufanya kazi katika kipindi cha siku chache kuanzia sasa. Mradi huu umeandaliwa na Mfuko wa Msamaria mwema, Shirika la Dawa na Sayansi la Gilead pamoja na Idara ya Afya, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Huduma hii inawalenga watanzania wote pasi na ubaguzi wa kidini wala mahali anapotoka mtu. Hii ni huduma ya kitabibu kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi na wale ambao bado hawajaathirika ili waweze kuchukua tahadhari kwa kujikita katika maadili na kanuni bora za afya na pale itakapoonekana inafaa, kuwasaidia maskini na watoto yatima.

Mradi huu kimsingi unajikita katika maeneo makuu manne katika utendaji wake: kuwezesha miundo mbinu ya ya sekta ya afya ambayo tayari inafanya kazi katika kuchunguza, kupima na kutoa tiba ya kurefusha maisha kwa wale walioathirika sanjari na kutibu magonjwa nyemelezi. Vituo vilivyoteuliwa ni Bugisi, Buhangija, Mija na Ngokolo.

Pili, Mradi huu utatoa huduma ya mafunzo maalum kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya kijamii na huduma za afya. Tatu, mradi huu utakuwa unatoa huduma ya elimu kwa wananchi hususan wanaoishi vijijini. Nne, ni kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma ya chakula kwa watoto na watu wazima walioathirika kwa virusi vya Ukwimwi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.