2015-04-30 10:14:00

Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya Tano ya Kipindi cha Pasaka


Tunaendelea kama kawaida yetu kutafakari Neno la Mungu, leo ikiwa ni Dominika ya V ya Pasaka mwaka B. Ujumbe wa Neno la Mungu ni mwaliko kwako kuwa tawi la mzabibu lizaalo matunda. Bwana ndiye mzabibu wa kweli nasi ni matawi yake.

Katika somo la kwanza toka kitabu cha Matendo ya Mitume tunapata simulizi juu ya Mtume Paulo jinsi alivyokuwa akiogopesha Jumuiya ya Mitume na wafuasi wengine. Wanamwogopa hapo mwanzoni kwa maana alikuwa mfitini mdhulumaji wa ukristu. Alikuwa mtesi nambari wanu, akiwatesa wafuasi wa Bwana katika Kanisa la mwanzo. Mara moja tunajifunza kuwa ubaya na madhulumu huleta woga na hofu katika jumuiya ya watu! Jambo la wasi wasi katika nchi yetu kwa sababu ya dhuluma linazidi kuongezeka, tumwombe Kristu Mchungaji mwema atuoneshe njia ya kuondokana na ubaya uliochanzo cha woga katika maisha yetu.

Wafuasi na Mitume hawataamini mpaka Paulo athibitishwe na Mt Barnaba. Ndiyo kusema nasi katika maisha yetu kuna wakati fulani tuna mashaka, au tuko katika safari ya wito, yatupasa kuthibitishwa na Mama Kanisa. Kumbuka pia katika maisha ya kiroho tunahitaji msindikizaji wa kututhibitisha mbele ya Kanisa na Mungu. Mtume Paulo akisha thibitishwa anasonga mbele na kuwa mtume wa mataifa. Katika utume wake daima atajiweka katika maongozi ya Bwana kwa njia ya Roho Mtakatifu akifanya daima mawasiliano na Mitume waliokabidhiwa wajibu wa kusimamia imani. Ndiyo kusema nasi tukishapokea utume kwa njia ya ubatizo au kwa njia ya sakramenti nyingine tunahitaji kila siku kwa njia ya sala kuthibitishwa na Kristu mwenyewe kwa njia ya Roho Mtakatifu tukiwa wana wa Kanisa na ndani ya Kanisa lake.

Katika Somo la pili toka barua ya Mt. Yohane, tunaona hoja kuu ni upendo unaojidhirisha kwa njia ya matendo huduma. Yaani imani iliyotendaji, iliyojaa fadhila ya kujitoa kwa ajili ya wengine. Anasonga mbele akitangaza neema za Mungu kwa wale watakaoshika amri za Mungu. Ni kweli, ni tendo jema na la upendo kushika amri za Mungu kama dira ya mapendo ya Mungu kwa mwanadamu.

Katika somo la Injili Mwinjili Yohane anakazia wajibu wa mkristu kukaa katika pendo la Baba. Anaweka mbele yetu picha ya mzabibu akisema Yesu ni mzabibu wa kweli nasi ni matawi yake. Anatudai kumbe kuwa matawi yanayozaa matunda maana yasiyozaa atayakata. Kabla ya kuzaa matunda lazima kubaki katika mwunganiko naye. Hivi leo Mama Kanisa atualika kubaki katika muunganiko naye kwa njia ya sakramenti, imani na mamlaka ya Kanisa. Na kwa jinsi hiyo tutakuwa tumebaki katika muunganiko na Kristu kwa maana Kristu ndiye kichwa cha Kanisa.

Kukaa nje ya Kanisa, au tuseme kutowajibika katika majukumu ya Kanisa ni kufa kiimani na matokeo yake ni kukauka na hatimaye Bwana atafyeka tawi hilo. Jiulize nini maana ya kufyeka au kukata. Na kama tawi limekauka si ni la kutumia kutengeneza moto? Basi jihadharini na chachu ya ulimwengu iletayo ukavu hasara kwa moyo na roho zetu.

Mpendwa nikutakie heri na mapendo Mungu, ubaki katika mzabibu wa kweli na hatimaye mwishoni ufurahie Pasaka ya Milele mbinguni. Tukutane siku na saa kama hii Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristo. Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.