2015-04-30 12:20:00

Mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Seychelles


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 30 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na Rais James Alix Michel wa Jamhuri ya Watu wa Seychelles, ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Mons. Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya viongozi hawa wawili, wamegusia mahusiano mema yaliyopo katika pande hizi mbili pamoja na kuangalia mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Seychelles hususan katika sekta ya elimu na afya. Baadaye wamejadiliana mambo msingi kwa kujikita zaidi katika utu na heshima ya binadamu; maendeleo endelevu pamoja na dhamana ya kulinda na kutunza mazingira. Baadaye wamegusia pia masuala ya kisiasa na kijamii nchini Seychelles na katika kanda husika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.