2015-04-30 06:59:00

Jifunzeni kutoka kwa maskini, kwani hawa ni amana na utajiri wa Kanisa


Kwa namna ya pekee, Wakristo wanapaswa kuwajali maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake, kwani maskini ni hazina na amana ya Kanisa katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko ameyasema haya katika ujumbe wake kwa njia ya video aliowatumia wasanii wa Jiji la Roma ambao wameandaa maonesho maalum kwa ajili ya kutafuta fedha ya kuchangia miradi ya huduma ya upendo na mshikamano kwa mji wa Roma.

Umaskini unaoneshwa na wasanii si jambo tu la kuigiza anasema Baba Mtakatifu bali ni uhalisia wa maisha ya watu wengi sehemu mbali mbali za dunia, hali inayojionesha hata Roma. Kuna watu wasiokuwa na makazi maalum, wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha; kuna makundi makubwa ya watu wanaopatiwa chakula na Caritas Roma, vinginevyo, watu hawa wangekufa kwa njaa mitaani. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shuleni ya maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu wa kawaida wanaopaswa kuonjeshwa upendo na kuthamini utu wao. Kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humo kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Wasanii wasaidie kuhamaisha tunu msingi za maisha  kama vile: upendo kwa Mungu na jirani; umoja na mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwamba, wao si mzigo bali ni shule makini kwa wazazi na watoto wao; umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo kati ya watu wake. Jimbo kuu la Roma limekuwa ni kielelezo cha upendo na mshikamano kati ya watu.

Hapa Kanisa linajivunia kuwa na viongozi ambao wamejisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, daima wakitenda kama Wasamaria wema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Laurenti, Shemasi na shahidi pamoja na Padre Luigi Di Liegro, muasisi wa Shirika la msaada  Roma, Caritas Romana bila kuwasahau watu wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini ndani na nje ya Roma. Katika shule ya upendo, watu wanatafura faraja, mahusiano, utu na  heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, anatamani kuona watu wengi zaidi wakijisadaka kwa ajili ya kuwaonjesha huruma na upendo maskini na wote wanaoteseka kiroho na kimwili; kuwakarimu wakimbizi na wahamiaji wanaosalimisha maisha yao kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma; kuwaonjesha tabasamu na furaha, wale wote waliokata tamaa na kupondeka moyo. Kanisa halina budi kuwa karibu zaidi na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.