2015-04-29 15:23:00

Nyongeza haiwezi kuzidi fungu, ukayaona wapi hayo?


Mzabibu na mkuyu ni mimea miwili ambayo Taifa la Waisraeli (Wayahudi) walijilinganisha nayo katika uhuasiano wao na Mungu. Wayahudi waljiona kama mzabibu uliostawi na kuzaa matunda yampendezayo Mungu kuliko mataifa mengine yote. Kwa maana hiyo pembeni mwa lango kubwa la hekalu la Yerusalemu kulining'inizwa kitu kama nondo ya dhahabu lililopondwa mithili ya tawi la mzabibu na kupambwa umbo kama la vitita vya zabibu za dhahabu. Wahaji waliofika kusali walibeba vitita halisi vya zabibu na kuvining’iniza juu ya tawi hilo la dhahabu. Dhahabu iliwakilisha ukuu na uzuri wa Mungu na zabibu ziliwawakilisha Wayahudi kama matunda mazuri yampendezayo Mungu. Hadi leo alama hiyo inawakilishwa na menorah, yaani kinara cha dhahabu chenye matawi sita. Kwa hiyo, Wayahudi walijiona wao wako damdam na Mungu na wao ndiyo uzao bora wa Mzabibu.

Kuhusu mahusiano hayo ya Wayahudi na Mungu, Nabii Isaya katika utenzi “Mpenzi na shamba lake la mizabibu” anaufananisha mzabibu huo na mpenzi yaani bi-arusi: “Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu….Kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza” (Isaya 5:1). Lakini Nabii anawakosoa Wayahudi kuwa wamegeuka kuwa mzabibu usiotoa matunda yampendezayo Mungu wala hayachangamshi au kuleta furaha kwa watu anaposema: “Mungu akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe alisikia kilio.” (Isaya 5:7).

Kumbe, mpenzi (mzabibu) wa Mungu umegeuka kuwa mdhulumu asiye na haki, analiza watu machozi. Akijitofautisha na mzabibu huo ulio chukivu kwa Mungu, Yesu anajitangaza mwenyewe kuwa: “Mimi ni mzabibu wa kweli.” Ili kuonesha kwamba hajajimilikisha mwenyewe shamba la mzabibu anakiri: “na Baba yangu ndiye mkulima.” Maana yake Yesu siyo mkulima na hata sisi ni matawi tu ya huo Mzabibu. Kwa hiyo kama tawi halitazaa matunda basi hiyo itakuwa imekula kwa Baba (mkulima) na kwa Mwana (mzabibu). Lakini kwa vile mkulima hatakubali kujiangusha, atafanya juu chini ili tawi lizae matunda. Kwa hiyo Yesu aliye mzabibu analitahadhalisha tawi likae sawasawa ndani ya mzabibu ili liweze kuzaa matunda kwani: “Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa na kila tawi lizaalo hulisafisha.”

Kumbe hapa yahusu harakati azifanyazo Mungu hadi mzabibu uweze kuzaa zabibu ili zitengenee divai nzuri. Kwa hiyo jambo la muhimu linalosisitizwa hapa juu ya mzabibu ni kuzaa matunda. Kuna baadhi ya miti ya matunda kama haizai, mashina yake yanaweza kufaa kwa mbao nzuri, au kuni, au walau kuchana boriti au lati na matawi yake yakawa chanja. Kadhalika yaweza kupasua kuni za kuota moto au kupikia chakula. Kumbe mzabibu ni mti pekee ambao una kazi moja tu nayo ni kuzaa zabibu. Kama tawi la mzabibu halizai, basi tawi hilo halifai wala kwa kuni za kuota moto na hata jivu lake ni chafu halifai wala kwa kutengeneza chumvi ya magadi, kama asemavyo nabii Ezekieli “Mwanadamu, mzabibu una sifa gani kuliko mti mwingine, au tawi la mzabibu lililokuwa kati ya miti ya msituni? Je, mti wake waweza kutwaliwa, ili kufanya kazi yoyote? Watu waweza kufanya chango kwa huo, ili kutundika chochote? … Tazama ulipokuwa mzima, haukufaa kwa kazi yoyote, isuze ukiisha kuliwa na moto, na kuteketea, je waweza kufaa kwa kazi yoyote?” (Ezekieli 15: 1, 5). Kwa hiyo endapo mzabibu hauzai matunda, basi mkulima atafanya mambo mawili: hatua ya kwanza, atayaondoa au kuyakata matawi yasiyozaa matunda, na hatua ya pili ni kusafisha au kuchenga matawi, kama inavyosemwa: “Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa na kila tawi lizaalo hulisafisha.”

Kuhusu hatua ya kwanza ni ile ya kuliondoa tawi lisilozaa haina maana ya kuwatenga wale wasiozaa matunda la hasha, kwani Mungu anawapenda watu wote, yaani yaonesha harakati aliyo nayo Mungu kwa kila mtu. Matendo ya upendo ndiyo utomvu wa uhai wa mkristu. Unapotengana na utomvu huo, tawi linakauka  na haliwezi kuzaa. Vikwazo vinavyozuia kutozaa matunda vyaweza kuwa utajiri, kutokusaidia walio katika matatizo, uvivu, nk.  Kasoro hizo zote husahihishwa na Baba.

Hatua ya pili ni kusafisha au kupalilia. Kusafisha huko siyo kuharibu, bali ni kutia uhai na kuufanya mmea upendeze na uwe na afya zaidi ya kuzaa matunda. Katika maisha ya maadili yamaanisha kutoa mwongozo, utaratibu, hata kuweka mipaka au kukataza, kuacha madoido na vikorombwezo visivyo na maana. Tunaambiwa pia kuwa Neno au Injili (Habari njema) ndiyo aina ya mkasi au kifaa kinachotumika kukata na kusafisha tawi: “Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno lililowaambia… Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.” (Yoh.15:3,7). Mungu anatusafisha kutokana na kasoro zinazotuzuia kupenda kwa njia ya maneno yake. Mungu anatutunza kama mzabibu, anatoa matawi yasiyo na maana yanayozuia kutoishi upendo.

Yesu anaendelea kusema “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu.” Neno hili “Kaeni” kwa Kigiriki “menein” linatokea mara arobaini katika Injili ya Yohane na maana yake ni kuonesha moyo na dhamiri yako iko wapi. Mwanzo wa Injili ya Yohane wanafunzi wawili walipomwuliza “Rabi unakaa wapi” (Yoh. 1:38), hawakutaka kumwuliza anuani ya mahala anakokaa, bali walitaka kujua moyo wake uko wapi. Hivi ndivyo anavyotutakia Kristu kubaki ndani yake na kuungana naye kabisa na kuwa damdam, yaani kuwa tawi la mzabibu halisi, “Mimi ni mzabibu wa kweli ninyi ni matawi.” Haijalishi nifanya nini au sifanyi nini, kwa mastahili yangu au hata kwa makosa yangu, mimi niko katika Yesu naye yuko ndani yangu kama Yesu anavyosema kuwa sisi tulioungana na Yesu tupo afi kwa njia ya Neno (Injili) lake: “Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.” Kumbe Neno la Injili linaingia na kusafisha takataka zote, utoto na kutokomaa kwangu hata uwongo ninaosema nk. Kisha linatufanya kuwa huru na wepesi kuruka na kwenda popote anakotupulizia Roho.

Kinachotakiwa kwetu ni kukumbuka kuwa Yeye yuko tayari ndani yako, na wewe ndani mwake na kwamba tunayo tayari nguvu ndani yetu, nguvu ile itokayo kwa Mungu, nguvu iliyojaa neema tele za kuzichota. Tunachotakiwa kufanya ni kuzibua mifereji au mishipa ili iweze damu au utomvu wa neema uweze kupita. Harakati hiyo ndiyo aliyokuwa nayo Paulo kwamba “Mtu akiwa ndani ya Kristu amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya.” (II Korinto 5:17). “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu.” (Wagalasia 2:20).

Ndiyo maana ya Jumuia ya Kikristo inakuwa kama tawi linalotoa matunda daima. Mungu Baba ametuaminisha kazi hii ya kuzaa matunda ndani yake. Kwa njia ya Kristo, utukufu wa Mungu unakuwa katika kuzaa  matunda mazuri na matamu. “Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana.” Kuna aina tatu za utamu wa tunda: Kuna utamu wa upendo, kuna utamu wa uhuru na kuna utamu wa hamasa. Huwezi kutoa upendo kama huna uhuru na furaha, na kama hakuna uhuru huwezi kuhamasika. Kwa hiyo upendo, uhuru na hamasa ni utomvu na matunda mazuri ya Mungu katika sisi.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.