2015-04-29 14:32:00

Kanisa lina tumaini kuona haki, amani na utulivu vinarejeshwa Nigeria


Askofu Oliver Dashe Doeme wa Jimbo Katoliki Maiduguri, Nigeria, eneo ambalo kwa muda wa mrefu limekuwa ni uwanja wa mashambulizi na vita inayoendeshwa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria, anasema, anatumaini kwamba, Rais mteule Muhammadu Buhari wa Nigeria, ataweza “kula sahani moja” na Boko Haram, ili kuweza kukidhibiti, ili amani na utulivu viweze kurejea tena nchini humo. Hivi karibuni, limegunduliwa kaburi la pamoja ambalo kuna idadi kubwa ya maiti zilizozikwa humo, karibu na mji wa Damasak.

Inakadiriwa kwamba, watu zaidi ya 400 walitekwa nyara na kikundi cha Boko Haram wakati kilipokuwa kinapambana na Jeshi la Nigeria pamoja na nchi jirani. Boko Haram inaendelea kupandikiza utamaduni wa kifo kwani Jeshi la Nigeria halifanikiwa kubomoa ngome yake, ndiyo maana haishangazi kusikia mashambulizi yanayoendelea kutendwa na Boko Haram ndani na nje ya Nigeria.

Askofu Oliver Doeme anasema kwamba, Rais mteule Muhammadu Buhari kati ya mwaka 1983 hadi mwaka 1985 alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kijeshi nchini Nigeria. Ni kiongozi mahiri katika medani za kijeshi na kwamba, wananchi wengi wa Nigeria wanaonesha matumaini yao makubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini humo. Baadhi ya wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahudumiwa nchini Cameroon wameanza kurejea tena nchini Nigeria na kwamba ,Askofu Doeme anaendelea kutembelea Parokia Jimboni humo, ili kuwafariji na kuwaimarisha watu kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kulipizana kisasi.

Boko Haram imefanya unyama mkubwa Jimboni Maiduguri kwani taarifa zinaonesha kwamba, kati ya Wakatoliki laki tano waliokuwemo Jimboni humo, waamini laki moja na ishirini na tano wameuwawa kinyama na Boko Haram. Waamini zaidi ya laki moja walilazimika kuyakimbia makazi yao, kati yao Mapadre ishirini na sita kati ya Mapadre Arobaini na sita walioko Jimboni humo. Miundo mbinu ya Parokia nyingi kwa sasa inakaliwa na wanajeshi wa Boko Haram. Shule tatu kati ya nne zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimboni humo, zimefungwa kwa lazima kwa kuhofia usalama wa wanafunzi na viongozi wao.

Askofu Oliver Doeme anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema ambayo kweli wameonja dhuluma na nyanyaso kubwa kutoka kwa Boko Haram, kushinda kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi na badala yake, wamwachie Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwalipia kisasi kwa wakati wake. Mungu peke yake ndiye hakimu mwenye haki, binadamu anaweza kukosea na kujikuta anatambukia kwenye maafa makubwa zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.