2015-04-28 15:59:00

UN: Inasubiri hotuba ya Papa Francisko na Waraka wake kuhusu Mazingira


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 28 Aprili 2015 amekutana kwa kitambo kidogo na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon ambaye amekuwepo hapa mjini Vatican kwa ajili ya kushiriki katika Warsha ya Kimataifa kuhusu utunzaji bora wa mazingira sanjari na heshima kwa utu wa binadamu kwa kuangalia mwelekeo wa kimaadili katika mabadiliko ya tabianchi pamoja na maendeleo endelevu.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali kuhutubia kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa hapo tarehe 25 Septemba, 2015 atakapotembelea nchini Marekani. Jumuiya ya Kimataifa pia inasubiri kwa hamu na matumaini makubwa changamoto na mwongozo utakaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake mpya wa kichungaji kuhusu Mazingira.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amefafanua baadhi ya majukumu yanayotekelezwa kwa sas ana Umoja wa Mataifa pamoja na changamoto ambazo wanakabiliana nazo kwa wakati huu hususan: athari za mabadiliko ya tabianchi, changamoto ya wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, vita pamoja na majanga asilia yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.