Baba Mtakatifu Francisko mapema Jumatatu 27 Aprili 2015, , akihutubia kikundi cha Maaskofu kutoka Benin Afrika Magharibi , alishukuru kwa huduma yao, yenye kuushuhudia upendo wa Kristo kupitia utendaji wamiradi mbalimbali ya Kanisa, nchini Benin. Na hivyo akawahimiza waendelee kutoa msaada katika maisha ya kiparokia, kuhamasisha idadi kubwa ya waamini kushiriki katika maadhimisho ya kanisa kwa moyo wa dhati na kufanya mabadiliko ya kiroho hasa kwa ajili ya miito na ukuzaji wa majadiliano kati ya dini . Maaskofu hao wako Roma kwa ajili ya ziara ya kitume ya ad limina Viist, wakiongozwa na Askofu Antoine Ganyè , Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Benin.
Baba Mtakatifu alionyesha pia kutambua changamoto halisi mfululizo wanazokabiliana
nazo Maaskofu na hasa matatizo makubwa yanayohusiana na masuala ya kifamilia. Alionyesha
tumaini lake kwamba, Sinodi ya Pili juu ya Familia itakayofanyika Roma Mwezi Oktoba
, itaweza jaribu kupata baadhi ya majawabu. Na hivyo aliwahimiza waendelee bila kuchoka
na jitihada za kusaidia familia, katika yote mawili kiroho na katika maisha ya kila
siku. Papa alionyesha kutambua kwamba ndoa ni moja ya wito mgumu katika maisha, kutokana
na hali halisi za kijamii na kiutamaduni. Na hivyo inakuwa ni hitaji la lazima kwa
viongozi wa Kanisa, kusaidia kuunda familia za kweli zilizosimikwa katika misingi
ya upendo wa kudumu, kwa kuwa familia daima ni ukweli, unaotakiwa na Mungu. Ndoa ni
zawadi kutoka Mungu mwenyewe ambayo huwaletea watu na jamii kwa ujumla furaha amani
na utulivu. Familia Papa alisema ni kitengo msingi cha jamii.
Aidha Papa alizungumzia changamoto nyingine inayowakabili Maaskofu wa Benin, kuwa
ni matatizo ya vijana na elimu, na hapohapo akatoa shukurani zake kwa juhudi zinazofanywa
na Kanisa nchini Benin ambako wameweza kufungua shule Katoliki nyingi katika majimbo
yao. Na hivyo akazungumzia umuhimu wa kukutana katika mazungumzo na tamaduni mbalimbali
za kidini, hasa na Uislamu. Na alishukuru kwa Benin , kuwa mfano bora wa maridhiano
kati ya dini , lakini pia akaonya kwa ajili ya kulinda urithi huo teke, umuhimu wa
kuwa macho kutokana na hali za kisasa za mwingiliano wa watu kimataifa.
Na hivyo, kupitia ukuzaji wa maelewano na haki katika Makanisa ya mahalia majimboni
mwao, unakuwa ni wajibu kwa Maaskofu, kuwa watendaji wakuu wa maendeleo katika nchi
yao. Pia Papa alikitazama kipeo cha uchumi wa dunia kinachoathiri mataifa mengi ,
akisema ni muhimu kutenda kinyume na wimbi la sasa , kuwa kinyume na utamaduni wa
ulaji , utamaduni wa kufuja mali ulioenea kila mahali kama ilivyoelezwa katika waraka
wa Injili ya Furaha (cf. Evangelii Gaudium, 53) na kusambaza maadili ya Injili ya
ukarimu na kukutana.
Papa aliendelea kuwakumbusha Maaskofu kwamba, huduma ya upendo ni utume wa Kanisa,
wenye kuunyesha asili yake , na hivyo alitoa mwaliko kwa watawa wote kuliishi hilo
kwa mkazo zaidi hasa katika mwaka huu wa maadhimisho ya Maisha yaliyowekwa wakfu ,
akionyesha pia kutambua majitolea ya ukarimu wa makuhani katika utumishi wa Injili.
Kwa namna hiyo alitoa maoni pia juu ya wingi wa miito ya Upadre Benin, kwa kuwataka
Maaskofu, kuwa na upendo wa kibaba kwa mapadre wao, na hasa kukuza ushirikiano
na udugu, ndani ya familia ya kikuhani na kutunza wale wanaohitaji, na kwa moyo
wa ukarimu kugawana utajiri wa rasilimali na makanisa mengine yenye kupungukiwa.Na
mwisho alihitimisha kwa kuonyesha kutambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Kanisa
na mamlaka za kiserikali . Na kwa sauti ya Kanisa kusikilizwa na kupendwa. Na hivyo
Papa aliwalika wote waendelee kushiriki katika maisha ya umma katika taifa lao na
ujenzi wa mahusiano bora zaidi kati ya makundi mbalimbali ya kijamii.
All the contents on this site are copyrighted ©. |