2015-04-28 10:04:00

Mh. Padre Edward Mapunda ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Singida


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa sana Padre Edward Mapunda kutoka Jimbo Katoliki la Singida kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Singida. Kabla ya uteuzi huu Askofu mteule Mapunda alikuwa ni mchumi wa Jimbo Katoliki Singida na Mratibu wa Idara ya Afya Jimbo Katoliki Singida.

Askofu mteule Edward Mapunda alizaliwa kunako tarehe 30 Septemba 1964, Mango, Jimbo Katoliki la Mbinga. Baada ya masomo ya Sekondari kwenye Seminari Dung’unyi, Singida, aliendelea na masomo kidato cha tano na sita kwenye Seminari ndogo ya Rubya, Jimbo Katoliki Bukoba. Akapata masomo ya Falsafa Seminari kuu ya Ntungamo iliyoko Jimbo Katoliki Bukoba na baadaye akahamia Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa masomo ya taalimungu.. Baada ya safari hii ndefu ya majiundo ya Kikasisi, tarehe 23 Novemba 1997 akapewa Daraja Takatifu la Upadre, Jimboni Singida.

Tangu wakati huo, Askofu mteule Edward Mapunda alifanya shughuli zifuatazo: Kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2000 alikuwa ni mlezi, Seminari Ndogo ya Dung’unyi. Mwaka 2000 - 2004 akajiendeleza kwa masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na huko akajipatia Shahada ya Uzamili katika elimu. Kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2006 alikuwa ni Makamu Gombera, Seminari Ndogo ya Dung’unyi na kuanzia mwaka 2006 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Singida alikuwa ni Mchumi wa Jimbo Katoliki Singida na Mratibu wa Idara ya Afya Jimboni.

Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki Singida ni sehemu ya Jimbo kuu la Dodoma ambalo lina ukubwa wa kilometa mraba 49, 341 na wananchi zaidi ya 1, 500, 000 na kati yao kuna Wakatoliki 238, 307. Jimbo Katoliki Singida lina Parokia 22 zinazohudumiwa na Mapadre wa 67 kati yao Mapadre 50 ni wa Jimbo na Mapadre 17 ni wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume. Jimbo lina watawa 423 na majandokasisi 14. Jimbo Katoliki Singida limekuwa wazi tangu tarehe 13 Januari 2013 baada ya Askofu Desiderius Rwoma kuteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.