2015-04-27 13:43:00

Papa aishukuru Uswiss kwa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 27 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza kwa faragha na Malkia Silvia wa Uswiss, aliyekuwa ameambatana na baadhi ya wanafamilia na watu waliokuwa kwenye msafara wake. Padre Federico Lombardi anabainisha kwamba, Malkia Silvia, Jumatatu anashiriki katika matukio mbali mbali yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Uswiss mjini Vatican, hususan kwenye Kongamano ambalo limeandaliwa na Taasisi za Kipapa ya Sayansi Jamii.

Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu “Biashara haram ya binadamu, hususan miongoni mwa watoto. Ametembelea Maktaba ya Kitume ya Kanisa Katoliki, ili kuzindua Deski la Ugawavi, ambalo limetengenezwa kwa msaada wa Mfuko wa Mfalme Gustavo Adolfo wa VI.

Malkia Silvia katika mazungumzo yake na Baba Mtakatifu amemwelekeza jinsi ambavyo Uswiss inayojikita katika kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Baba Mtakatifu ameishukuru Serikali ya Uswiss kwa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Malkia Silvia amemzawadia Baba Mtakatifu Francisko kitabu cha sala kwa watoto, kuonesha jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele kuwahudumia watoto wake katika maisha ya kiroho, ili waweze kuwa wema na wanyofu, jambo ambalo Baba Mtakatifu amempongeza kwa dhati kabisa.

Baba Mtakatifu amepata pia fursa ya kuzungumza na Malkia Madeleine aliyekuwa ameambatana na mme pamoja na mtoto wao wa mwaka mmoja anayejulikana kama Leonore. Baba Mtakatifu amezungumza nao kwa kina na mapana, huku wakibadilishana mawazo na mang’amuzi ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.