2015-04-27 09:57:00

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu: Imarisheni huruma!


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Kutoka ndani ya hazina ya Mama Kanisa tunaendelea kukuletea  ujumbe kutoka katika Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Fransisko, kwa nafasi ya maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Barua yetu yenye kichwa cha habari kisemacho “Misericordiae Vultus” yaani Uso wa Huruma, ni mwaliko kwetu sote kutafakari kwa kina na mapana juu ya huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu.

Ni rai kwetu sote, katika unyonge na udhaifu wetu, kuikimbilia huruma ya Mungu, ili Mungu wetu mwenye huruma atusafishe, atuinue, atujaze neema zake. Ni kwa huruma yake kuu, daima anatumiminia wingi wa neema zake katika mazingira mbalimbali na kwa namna mbalimbali. Ni jukumu letu, kila mmoja wetu kwa namna yake, kushirikiana na neema hizo za Mungu, ili zitupatie mafaa ya wokovu. Mungu hutujalia neema hizo, kwa Uradhi wake, kwa huruma yake na kwa ukarimu wake mkuu. Ni sisi kwa uhuru wetu, tunachagua kushirikiana na neema hizo za Mungu. Tukiifungua mioyo yetu, na kumpa Mungu nafasi; tukiyaweka maisha yetu mikononi mwake, ili yeye atende na atukuzwe katika maisha yetu, hapo tutauona mkono wa Bwana, tutaonja uwepo wake na  kazi yake katika maisha yetu.

Katika kipindi kilichopita, mpendwa msikilizaji tulitafakari jinsi Mungu wetu anavyomwilika katika Kristo wake. Na tukaona pia jinsi Kristo Yesu alivyo kioo cha Huruma ya Baba, na jinsi ambavyo sisi tunaoshirikishwa maisha, utume na mafumbo ya Kristo tunavyoshirikishwa huruma ya Mungu; na kwa hayo yote mwishoni tukaalikwa kuiambata Huruma kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo na huruma. Leo tuendelee kwa kuutazama mwaliko wa kuimwilisha huruma hiyo ya Mungu.

Mantiki yake ni hii: Sisi tunapokea huruma ya Mungu kila siku. Na huruma hiyo ya Mungu tunashirikishwa sio tu kwa ajili yetu bali kwa ajili ya jirani zetu pia. Ili kuweza kuwafikia binadamu wenzetu na kuwaonjesha huruma hiyo ya Mungu, ni lazima kuwa tayari kuishi katika uhalisia wa sasa; kuepuka kishawishi cha kujivua fahamu, yaani kuishi kana kwamba huoni wala husikii kilio cha jirani, kuishi kana kwamba hujui kuwa wewe ni mjenzi wa leo na kesho iliyo njema. Tusijivue fahamu! Tunaalikwa sote, kuishi na macho yanayoona na kutazama, kuwa na masikio yanayosikia na kusikiliza, kuwa na mdomo unaozungumza na kusema, kuwa na miguu inayotembea na kwenda, kuwa na akili inayowaza na kufikiri namna ya kujenga hali njema kati ya watu; zaidi – zaidi tunaaliwa  kuwa na moyo unaoonja, kupokea na kutoa huruma ya Mungu.

Ni katika mtazamo huo mpendwa msikilizaji, Baba Mtakatifu Fransisko ndani ya Misericordiae Vultus yaani Huruma ya Mungu, anatutafakarisha juu ya sura ya Yesu wa Huruma, anayewaona makutano waliyomfuata ili kumsikiliza, anawatazama na kuona kuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasiokuwa na mchungaji na anawaonea huruma (rej. Mt 9:36). Ni katika mtazamo huu wa upendo wenye huruma aliwaponya wagonjwa walioletwa kwake (rej. Mt. 14:14), na kwa mikate michache na samaki anaulisha umati mkubwa wa watu (rej. Mt.15:37). Baba Mtakatifu anakaza kusema, kilichomsukuma Yesu kutenda hayo yote sio kingine bali ni huruma yake kuu. Ni kwa huruma aliweza kusoma  mioyo ya watu na akajibu vilio vya mioyo yao.

Mpendwa msikilizaji, hazina hii ya mafundisho ya Mama Kanisa inatutafakarisha kwamba, huruma ni ufunguo unaotufanya tufungue mioyo na maisha ya wenzetu na tuweze kusoma vilio vyao na kuwasaidia. Mtu mwenye huruma ni rahisi zaidi kuona, kuwafikia na kuwagusa wenzake katika mahangaiko yao na hivyo kuwashirikisha huruma yenye upendo, huruma inayofariji, huruma inayoinua, huruma inayotia moyo na matumaini, huruma inayofukuza giza katika maisha. Katika maisha yetu hatuhitaji kuwa na  mambo makubwa sana ili  kuimwilisha huruma ya Mungu kwa binadamu wenzetu. Tumtazame Kristo, kioo chetu ambaye ni kwa mikate michache na samaki wachache anaushibisha mkutano mkubwa sana, wanakula na kusaza.

Ndivyo mini na wewe tunavyotumwa leo! Hutuhitaji kuwa na mali nyingi sana au mamillioni ili kuweza kutenda matendo ya huruma na upendo kwa wenzetu. Tunaweza tukawa na mali zote na mzigo wa fedha za kila aina, lakini kama hatuna huruma, hatutamfaa yoyote wala sisi mwenyewe. Ndiyo; mali inaweza kuwa inahitajika pia, lakini kabla ya mali kwanza itangulie huruma, huruma yenye upendo. Ni hapo tu, hiyo mali itakuwa ni kitendea kazi cha huruma. Mapaji tuliyo nayo, tukiyatumia kwa huruma ya upendo, tutaugusa umati mkubwa wa watu, na kwa njia hiyo, tutawaonjesha watu huruma, wema na upendo wa Mungu.

Kila mmoja wetu kwa huruma ya Mungu amejaliwa mikate michache na samaki wachache (kiasi gani, hiyo ni siri ya Mungu). Ila kwa uhakika kila mwanadamu, anayo mikate michache na samaki wachache. Mikate na samaki hao wanamwilika katika afya zetu, nguvu zetu, karama zetu, mali zetu halali, elimu, huduma mbalimbali za kitaaluma na mambo kadha wa kadha. Hayo uliyonayo, ukiwashirikisha wenzako kwa huruma na upendo, hakika utawagusa umati mkubwa na wewe bila kutindikiwa kamwe. Kinachotakiwa ni kufungua macho kwa huruma, kuona na kutazama kisha kutenda kwa upendo. Ni hapo tu, tutakuwa tunaimwilisha huruma ya Mungu katika maisha yetu. Dunia yetu sasa inahitaji watu wenye huruma zaidi. Ni mimi na wewe, tutaweza kupunguza vilio vya familia ya mwanadamu. Na tukitaka, tunaweza Asante kwa kuisikiliza radio Vatican. Usisahau kusali Rozali ya Huruma ya Mungu, ili atuhurumie sisi na dunia nzima.

Kutoka Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.