2015-04-27 14:03:00

Kanisa Katoliki nchini Namibia: Bega kwa bega na maskini na wanyonge!


Askofu mkuu Liborius Nashenda, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Namibia na Lesotho wakati huu wa hija yao ya kitume inayofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano anabainisha kwamba, Kanisa limebahatika kuwa na Wakristo wengi katika nchi hizi mbili. Ni nchi ambazo pia zinakabiliwa na matatizo, changamoto na fursa ambazo zikifanyiwa kazi zinaweza kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watu: kiroho na kimwili. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, Kanisa nchini Namibia na Lesotho linajitegemea kwa rasilimali watu na fedha, ili kuliwezesha kutekeleza dhamana na utume wake kwa ufanisi na tija.

Waamini walei wanaendelea kujengewa uwezo ili wajisikie kuwa ni sehemu muhimu sana katika kujenga, kuliimarisha na kulitegemeza Kanisa la Kristo, sanjari na kusaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, ili kweli Namibia na Lesotho, ziweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Changamoto ya pili ni kuhakikisha kamba, Kanisa linahamasisha, linapalilia na kukuza miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwa namna ya pekee wito wa: Upadre na maisha ya kitawa, kwani kwa sasa kuna upungufu mkubwa wa miito hii ndani ya Kanisa.

Hapa anasema Askofu mkuu Nashenda, Kanisa linapenda kuwekeza zaidi kwa vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa, ili kweli waweze kuwa ni watakatifu, wema na wachapakazi; vyombo makini vya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linaendelea kufanya maboresho makubwa katika nyumba za malezi na taasisi za elimu Katoliki ili ziweze kutekeleza dhamana na utume wake kwa ufanisi mkubwa.

Majiundo makini na endelevu kwa Familia ya Mungu Namibia na Lesotho ni uwanja mwingine ambamo Kanisa linaendelea kulifanyia kazi kwani kuna ongezeko kubwa la waamini walei wanaopaswa kufundwa barabara ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa kuanzia katika familia. Huu pia ndio mwelekeo wa Kanisa kwa ajili ya Wakleri na Watawa; kwani kwa pamoja wakiungana wanaweza kuendeleza kazi kubwa ya Uinjilishaji mpya, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kanisa katika mapambano ya kudai uhuru, limejipambanua kwa kuwa kati ya watu na kwa ajili ya maskini na wote waliokuwa wanakusukumizwa pembezoni mwa jamii. Limefanya kazi bega kwa bega na wananchi wa Namibia kwa muda wa miaka 25, umri wa mtu mzima kabisa. Kanisa halikujihusisha na mambo ya kisiasa, bali liliwajengea wananchi uwezo wa kusimama kidete kutafuta, kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu, hadi kunako mwaka 1990, Namibia ilipojipatia uhuru wake.

Baada ya kujipatia uhuru, Kanisa likaendelea kushiriki katika mchakato wa kusaidia kuwarudisha wananchi wa Namibia waliokuwa wamekimbilia uhamishoni huko Angola, Zambia, Zimbabwe na sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa limeendelea kuwa mdau mkuu wa mikakati ya maendeleo endelevu kwa njia ya huduma makini katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Kanisa likajifunga kibwebwe kupambana na umaskini na majanga mbali mbali yanayokwamisha maendeleo ya watu. Kwa hapa kwa hakika anasema Askofu mkuu Nashenda, Kanisa linamshukuru Mungu kwa mchango wake katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Namibia.

Kanisa linaendelea kuchangia mawazo na mikakati kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa pia linaendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuimarisha umoja, maridhiano na mshikamano wa kitaifa; utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.