2015-04-27 09:06:00

Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu: Tovuti ya habari, tafakari na picha


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuzindua rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu hapo tarehe 8 Desemba 2015, kama kumbu kumbu ya kuhitimishwa rasmi maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Uzinduzi huu utaambatana na kufunguliwa kwa lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kutokana na umuhimu wa tukio hili, Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, hivi karibuni limezindua tovuti maalum kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei kuu ya huruma ya Mungu inayotumia anuani ifuatayo: www.iubilaeummisericordiae.va

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amelikabidhi Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya, dhamana ya kuratibu maadhimisho haya, ili kuwasaidia waamini wengi kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao. Katika tovuti hii maalum, kutakuwepo na tafajari, mahubiri, taarifa pamoja na picha mbali mbali zitakazokuwa zinachukuliwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Hapa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaotaka kujitajirisha kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu wanaweza kufanya hivi na kwamba, kuna mwingiliano wa karibu na taarifa mbali mbali zinazotolewa na Gazeti la L’Osservatore Romano na Radio Vatican kuhusiana na mchakato wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Hizi ni taarifa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.