2015-04-26 10:47:00

Yesu ndiye mchungaji mwema anayejisadaka kwa ajili ya Kondoo wake!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi 19 alisali sala ya Malkia wa mbingu pamoja na waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 26 Aprili 2015, Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema. Mapadre wapya wawili wameshiriki pamoja na Baba Mtakatifu Francisko kutoa baraka yao ya kwanza kwa waamini waliokuwa wamefurika kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kuitafakari Injili ya Jumapili hii katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kristo kweli ni mchungaji mwema anayejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Yesu Kristo mchungaji mwema ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo alioano kwa ajili ya Kondoo wake, kiasi cha kuyatoa maisha yake ili yawe ni sadaka, anayetafuta mafao ya wengi na kushiriki katika mchakato wa maisha ya kila siku na daima yuko tayari: kuwaongoza, kuwalisha, kuwalinda na kuwatetea kwa gharama ya maisha yake binafsi. Yesu ndiye mchungaji mwema, mkweli na mwema, anayedhihirisha upendo wa Mungu kwa binadamu, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini kutambua na kuithamini zawadi hii.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kutafakari na kushuruku, hakutoshi, kwani waamini lazima wajibidishe kumfuata Mchungaji mwema, lakini kwa namna ya pekee, wale ambao wamepewa dhamana hii na Mama Kanisa. Hawa ni Wakleri wanaopaswa kuwa ni mfano wa huduma pasi na kumezwa na malimwengu, huku wakiendelea kumuiga Yesu aliyeacha yote ili kumkomboa na kumshirikisha mwanadamu huruma ya Mungu.

Hiki ndicho kielelezo cha maisha na utume kwa Mapadre wapya 19 watakaotoa huduma kwa Jimbo kuu la Roma; Mapadre waliopewa Daraja Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 52 ya Kuombea Miito Duniani. Bikira Maria awasaidie Wakleri wote ari na moyo wa huduma kwa Familia ya Mungu, kwa kuwatangazia Injili kwa moyo wa furaha; kwa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji na kwa njia ya mfano wa maisha yao, waamini wapate kweli wachungaji wema na watakatifu.

Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, amewakumbuka na kuwaombea wananchi wa Nepal, India, Bangaladesh na Tibet ambao wamekumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wote hawa waonjeshwe mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Maria Elisa Turgeon, Mama Mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Mama Yetu wa Rozari Takatifu wa Mtakatifu Germano. Mwamke ambaye ni mfano wa kuigwa, aliyejikita katika sala na malezi kwa watoto wadogo. Ni mfano wa maisha ya kuwekwa wakfu kwa Mungu na huduma makini kwa jirani.

Mama Kanisa anafanya pia kumbu kumbu ya Mwaka mmoja, tangu Yohane Paulo II alipotangazwa kuwa Mtakatifu, tukio ambalo limeadhimishwa sehemu mbali mbali za dunia, changamoto kwa waamini ni kuendelea kumfungulia Kristo malango ya maisha na mioyo yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.