2015-04-26 14:12:00

Siku ya kuombea Miito Duniani: Maisha yenu yawe ni ushuhuda wa imani


Yesu Kristo ndiye Kuhani mkuu kadiri ya Agano Jipya na kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanashiriki Ukuhani wake, lakini Mapadre wanatekeleza dhamana hii kwa ajili ya Familia yote ya Mungu, ili kuendeleza utume wa Yesu unaojionesha kwa namna ya pekee kama: Mwalimu, Kuhani na Mchungaji mwema. Yesu alitumwa kutekeleza dhamana hii na Baba yake wa mbinguni, utume ambao umeendelezwa na Mitume pamoja na waandamizi wao na hatimaye, Mapadre, wanaoitwa katika huduma kwa ajili ya Watu wa Mungu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema na Siku ya 52 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu ametoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi 19 kutoka Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu anasema Mashemasi hawa wametafakari kwa kina na mapana kabla ya kujongea Altareni mwa Bwana, ili kuwekwa wakfu kuwa Mapadre. Hii ni hatari kubwa kwa wao wenyewe, Maaskofu na Mwenyezi Mungu.

Hawa ni Mapadre ambao wamewekwa wakfu tayari kuungana na Askofu wao ili kutangaza Injili, kuhudumia Mafumbo Matakatifu ya Kanisa, Kuongoza Watu wa Mungu, lakini zaidi, watakuwa ni waadhimishaji wakuu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha sadaka endelevu ya Kristo Msalabani. Kwa njia hii wanakuwa pia ni washiriki wa utume wa Kristo, Mwalimu na Bwana. Wanatumwa kuwatangazia Watu wa Mungu Injili ya Furaha waliyoipokea wao wenyewe, lakini kwanza kabisa wanapaswa kuisoma na kuitafakari, tayari kuimwilisha katika ushuhuda wa imani tendaji.

Neno la Mungu anasema Baba Mtakatifu ni lishe tosha kabisa ya maisha ya kiroho. Mahubiri yao yasaidie kufungua mioyo ya waamini, kwa vile ni mahubiri yanayobubujika kutoka katika undani wa ushuhuda wa maisha yao. Mafundisho ya Kanisa ni chemchemi ya furaha kwa waamini na manukato ya ushuhuda wa imani inayojenga na kuwaimarisha waamini. Mapadre wanatumwa kuendeleza kazi ya kuwatakatifuza waamini, kwani sadaka yao inaunganishwa na ile Sadaka ya Kristo Msalabani.

Kwa njia ya mikono yao mitakatifu, Mapadre wapya wataweza kuadhimisha kwa ibada na uchaji Mafumbo Matakatifu ya Kanisa. Waendeshe Ibada kwa moyo wa unyenyekevu pasi na haraka, kwani kwa njia ya maadhimisho haya, wanashiriki katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo na hivyo kukirimiwa uwezo wa kutembea pamoja na Yesu katika upya wa maisha.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wataliwezesha Kanisa kupata watoto wapya na kamwe wasimnyime mtu, Sakramenti ya Ubatizo, anapowaendea. Kwa Sakramenti ya Upatanisho, watawaondolea watu dhambi zao kwa jina la Kristo na Kanisa. Wawe ni Mapadre wanaonesha uso wa huruma ya Mungu, kwa kusamehe na wala si kuhukumu. Kwa mafuta matakatifu, watawafariji wagonjwa na kwamba, ili kutekeleza vyema dhamana na utume wao, hawana budi kuwa ni watu wa Sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu na kwa njia hii , watakuwa kweli ni sauti ya Watu wa Mungu na ulimwengu katika ujumla wake.

Mapadre watambue kwamba, wameteuliwa miongoni mwa watu kwa ajili ya mambo matakatifu, kumbe Familia ya Mungu inatarajia kuona mambo matakatifu, mafumbo ya Kanisa yanayoadhimishwa kwa furaha na huduma ya upendo inayotolewa kwa kuiga mfano wa Kristo Mchungaji mwema. Padre ajitahidi daima kuwa ni mtu wa watu kwa ajili ya watu.Mapadre wanashiriki utume wa Kristo, kiongozi na mchungaji mkuu, huku wakiwa wameungama na Askofu wao, kielelezo cha umoja na mshikamano wa Familia ya Mungu ndani ya Kanisa. Lengo ni kuwasaidia waamini kumwendea Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo na Roho Mtakatifu. Daima mbele ya macho yao, wajitahidi kumwona Kristo Mchungaji mwema, aliyekuja ili kuhudumia, ili kuwaganga na kuwaokoa wale waliopotea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.