2015-04-25 08:57:00

Wito ni safari ya kutoka ndani ya nafasi kwenda kwa Mungu na maskini


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa siku ya 52 ya kuombea miito ndani ya Kanisa anasema wito ni safari kutoka ndani ya nafsi kwenda kwa Mungu na maskini. Tunasukumwa na haja ya kusali  kama Bwana alivyotualika katika- Lk. 10:2 akawaambia, mavuno ni mengi, lakini wafanya kazi ni wachache, basi, mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke wafanya kazi katika mavuno yake. Yesu anaonesha hitaji la kutumwa, wale wanaoitwa wanatumwa kwa ajili ya misioni – Lk. 10:1-16. Kwa ukweli, asili ya kanisa ni la kimisionari – Vat. II, Decr. Ad Gentes, 2). Chanzo cha wito ni katika kusikiliza sauti ya Kristo Mchungaji mwema. Ni kumruhusu Roho Mtakatifu atuingize katika mpango huu wa kimisionari, akituhimiza kutolea maisha yetu na kuyatumia kwa ajili ya ufalme wa Mungu.

Kujitoa maisha katika mtazamo huu, kunawezekana tu kama tunaweza kutoka ndani ya nafsi zetu.  Ndiyo tafakari yetu ya leo – kutoka ambako ndiyo wito wetu, ndiyo mwitikio wetu kwa mwaliko wa Mungu.  Sote tunajua kuwa neno kutoka linachukua nafasi gani katika Biblia na katika historia ya ukombozi. Katika kutoka toka utumwani kwenda kwenye uhuru wa watoto wa Mungu – taifa la Israeli linakombolewa. Hii ni kazi ya wokovu – Efe. 4:22-24 – imewabidi kuacha mwenendo wenu wa kwanza na kumwondosha mtu wa zamani mwenye kuharibika kwa kufuata tamaa potovu. Imewapasa kuwa watu wapya katika roho na maoni yenu. Mkamvae mtu mpya aliyeumbwa mfano wa Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.  Ni matembezi ya roho ya kikristo na kanisa zima, ni kujielekeza wazi kwa Mungu Baba.

Katika mzizi wa wito wa kikristo, kuna mwelekeo wenye msingi katika imani – kuamini inamaanisha kujitoa, kutoka katika mazingira yetu na ugumu wetu na kuelekeza maisha yetu kwa Kristo, kuwa Abrahamu aliyeacha nchi yake na akaingia katika matembezi yenye matumaini, akijua kuwa Mungu atamwonesha kuelekea njia mpya. Ye yote anayejiweka katika mpango wa Kristo wa ukombozi – atapata uzima wa milele kama asemavyo Yesu – Mt. 19:29 – na kila aliyeacha nyumba au kaka au dada au ndugu au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili ya jina langu, atapewa mara mia na hatimaye kuurithi uzima wa milele. Msingi wa haya yote ni upendo. Kwa hakika wito wa kikristo, msingi wake ni upendo unaovuta na kutuma kwenda zaidi ya kile kilichopo.

Ufahamu huu wa wa kutoka (exodus) ni mpango wa maisha ya kikristo na kwa namna ya pekee anayepokea wito wa kumtumikia Injili. Ni maisha ya kifumbo – fumbo la Pasaka. Wito daima ni lile tendo la Mungu anayetufanya tutoke katika hali zetu, unatufanya huru na kila aina ya utumwa, inatutoa katika mazoea ya ubinafsi na kutuelekeza kuelekea furaha ya kuunganika na Mungu na watu wake. Kujibu wito wa Mungu, ni kumwacha Yeye atutoe toka hali zetu na kuingia katika matembezi na Kristo, mwanzo na mwisho wa maisha yetu na furaha yetu.

Huu mpango wa kutoka unahusisha si tu mtu mmoja, bali tendo zima la kimisionari na uinjilishaji wa kanisa zima. Kanisa ni aminifu kwa Bwana wake katika mtazamo huu wa kutoka. Na yote yanayofanyika si kwa ajili yake tu na muundo wake n.k. Kinachotakiwa ni kutoka na kukutana na watoto wa Mungu, katika hali zao na kushiriki mahangaiko yao. Mungu anatoka katika hali yake na kukutana na  watu wanaoteseka na kuwapatia uhuru – Kut. 3:7 – Bwana akasema, mimi nimeona, nimeyaona mateso ya watu wangu wanaokaa Misri. Nimesikia kilio wanachotoa sababu ya wasimamizi wao wadhalimu. Kweli, nayajua mateso yao. Ndiyo namna hii ya uwepo wetu na kutenda na kanisa pia hutuita kuishi hivyo. Kanisa linaloinjilisha hukutana na mwanadamu, hutangaza neno la ukombozi, hutunza kwa neema ya Mugu waliojeruhiwa kimwili na kiroho, huwatuliza maskini na wahitaji.

Huu mpango wa ukombozi, humkamilisha pia mwanadamu. Kusikia na kulipokea neno la Mungu si tu swala binafsi. Si tu swala la kujisikia, bali ni wajibu, uwazi na ukamilifu unaokumbatia maisha yetu na kujitoa kwetu katika ujenzi wa ufalme wa Mungu. Hivyo wito wa kikristo, uliojengwa ndani ya moyo wa Baba, hutusukuma kuwajibika kwa ajili ya ndugu na maskini. Mfuasi wa Kristo huwa na moyo angavu uliofungwa katika ushirika wa kimisionari – Evangelii Gaudium, 23.

Injili ni Neno linalookoa, hubadilisha na hukamilisha maisha yetu. Tumpe Mungu nafasi katika maisha yetu, tulishike Neno lake, tujiweke katika njia ya Bwana, tuabudu fumbo lake tukufu na katika kuwatumikia wengine.Tuongozwe daima na Mama Bikira Maria, ambaye ni mfano halisi wa wito wetu. Hakuogopa kutangaza utayari wake – FIAT – katika kuitikia wito wa Mungu Baba. Yeye hutuongoza na kutulinda. Kama yeye tusiogope, ila tuwe tayari kujitoa kwa mapenzi yake Mungu – Lk. 1:39.

TUMSIFU YESU KRISTO.  PD. REGINALD MROSSO, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.