2015-04-25 14:36:00

Uhuru wa mtu katika maisha mchanganyiko kifamilia -


Katika Jumapili hii ambayo ni Jumapili ya kuombea Miito , Dunia Mama pia anapenda kuwazamisha katika tafakari ya kina,  nini maana na msingi wa uhuru kamili wa mtu katika maisha mchanganyiko ndani ya familia na jamii kwa ujumla. 

Watalaam wa sayansi ya jamii , wanasema ,  ni vigumu kuwa na maisha yenye furaha kamili iwapo  mtu hana uhuru kamili katika kuzungumza na kutenda. Lakini pia  wanaonya uhuru usiokuwa na mipaka , ni wendawazimu.  Kumbe kuna mawili ya kuzingatia, kuishi kama tunavyopenda, lakini wakati huohuo tunabanwa na wegine kwamba ni lazima kuheshimu kikamilifu uwepo wao. Uhuru hautangamani na uadilifu iwe ndani ya familia au katika maisha ya kijamii. Kila tendo ni lazima liheshimu wengine. Kutofanya hivo ni kuishi kinyume na amri kuu ya kwanza ya Mungu, "Mpende Mungu wako kwa moyo wako wote na  mpende mwenzako kama unavyojipenda mwenyewe".  Maana yake Mungu ni upendo na hivyo mtendee mwenzako kama unavyopenda kutendewa nae.  Huo ndio uhuru kamili, iwe ndani ya familia, kazini, mashuleni, mashambani, mijini, katika kumbi za michezo, n.k

Mpendwa msikilizaji , katika kuichambua mada hii ya uhuru wa mtu, sina  shaka sote tunakiri kwamba ,  ni haki kwa kila mwanafamilia kutambua haki zake na  asilia aliyoumbwa nayo, kama sehemu ya utu wake isiyoweza kutenganishwa nae. Na huo ndiyo msingi wa uhuru, haki na amani duniani. Na uhuru na amani  ya dunia huanzia ndani ya nyumba zetu wenyewe, na kusambaa kama nguvu ya joto la moto katika makandokando yake.  Mtu anayeishi kwa  uhuru  na  amani katika familia yake,  ni vigumu sana kuwa mtu mgomvi kwa watu wengine. Vivyo hivyo kwa mtu mwenye kujua maana ya uhuru wake , ni vigumu sana kudhulumu uhuru wa wengine. Mtu adilifu hutambua kwamba , kupuuza au kudharau haki na uhuru wa wengine , ni  kuibua matendo maovu dhidi ya wengine.  Ni kuzua kilio cha dhamira  na matarajio ya mtu katika kufurahia uhuru wake kimaisha, iwe katika kujieleza au kiimani. Ni kilio cha uhuru dhidi ya hofu na wasiwasi na ni kunyimana raha.  

Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika waraka wake "Fadhila katika Ukweli"  Sura ya 4, ambamo amezungumzia Maendeleo ya watu, haki na wajibu na mazingira , ameeleza kwa kina juu ya dhana  hii kwamba haki inahusiana na kuwajibika.  Papa anaonya kwamba,  mtu kuzingatia sana haki zake kunaweza  leta hatari ya kuona kama vile wengine hawana haki isipokuwa yeye peke yake, na hivyo kudai  kutendewa haki na wengine au mamlaka ya umma kama vile, ni yeye peke yake  mwenye  kuwa na haki za ziada kulliko wengine, kumbe binadamu wote kimsingi wana haki sawa.  Kuwa na mawazo kama ya kuona tu upande mmoja, kuwa na haki na wengine kama vile hawana ni dhana potofu yenye kudhoofisha hata haki za msingi na hivyo kusaba bisha ukiukaji wa haki. Papa Mstaafu Benedikto katika waraka huu, anasisitiza kuwa haki  msingi ni salama tu pale kila   mtu anapo pokea kama ni wajibu kuheshimu uhuru na  maendeleo ya watu wengine kama ni haki yao.  Papa anarudia kutaja  majukumu ya serikali,katika kuhakikisha kila jitihada inafanyika kwa ajili ya  kuhakikisha mahitaji ya maadili kwa wananchi yanatimizwa kupitia mifumo ya  kukuza maisha adilifu, kupitia mifumo mbalimbali kama dini na elimu na uchumi, ili mipango na utendo wote uwe kwa  ajili ya manufaa ya wanafamilia wote na jamii kwa ujumla.

Katika mapana yake, Papa anaona uwajibikaji huu unaopaswa  kufanyika kwa uhuru kamili wa mtu , wenye kushikamana  na wajibu wa kulinda uhuru na haki za wengine,  na hivyo kwa asili yake mtu hapaswi kujioni yeye ni wa muhimu  zaidi ya mwanadamu mwingine. . Daima akili ya mtu inapaswa kukumbuka kwamba binadamu wote tumeumbwa sawa kwa sura na mfano wa Mungu.  Utendaji wowote ule na maendeleo  ya mtu hayawezi kupunguza hadhi hiyo.

 Na ndivyo, pia Papa Mstaafu Benedikto,  alivyoeleza katika sura ya tano ya waraka wa Fadhili katika upendo ,  umuhimu  wa watu kuishi katika ushirika na kila mmoja. Anaeleza , kipimo safi cha  maendeleo ya watu, hutegemea juu ya yote,  utambuzi kwamba binadamu ni familia moja. Papa ameonyesha kujali kwamba, maisha ya kutengana,  husababisha uwepo wa matabaka tabaka , wenye kuwa navyo na wasiokuwa navyo na hivyo  hukuza umaskini kwa wengine. Kubezana kunakotokana na hadhi za vitu,  hujenga  utengano wa mtu kujisikia hastahili kuwa sehemu ya kundi fulani, na hivyo hujenga hali ya upweke, mwenyewe kujiona hafai katika kundi hilo la kijamii. Papa anataja dawa katika hilo,  ni ujenzi wa mshikamano na udugu kwa watu wote. Kila mmoja ajione kuwa ni sehemu ya jamii, kila mmoja ana kitu anachoweza kutoa kwa uhuru  wake kamili kwa wengine  kama jambo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wote.  Hakuna binadamu asiyekuwa na mchango wa thamani kwa wengine.  Hata ule uwepo wake tu ni lulu kimaisha . Aidha Papa Benedikto anaongeza  na kuhimiza   mshikamano wenye kuwa makini katika kujali mahitaji ya wengine. Ni  daima kutambua kwamba ,  tuna uwezo tofauti katika utendaji wetu. Kila mmoja ana kipaji chake katika mambo fulani kwa kadri alivyojaliwa na kudra.  Na ndiyo maana ya kila mmoja anapaswa kumheshimu mwingine kwa jinsi alivyo, kwa ajili ya kuwa na maisha bora yaliyosimikwa katika usawa na ushirikiano kwa ajili ya ustawi wa wote.  Papa Bendikto alieleza na kutahadharisha juu ya ubabe wa kidini na utamaduni  unavyoweza hatarisha  uhuru wa wengine kidhamira hasa uwepo wa imani tofauti,  katika kukuza ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya binadamu.  Papa  anasema,  utambuzi unahitajika ili watu waweze  kuepuka itikadi hatari na dini zenye kuhamasisha watu kukataa wengine walio tofauti nao.   Anasema dini lazima ishiriki katika  majadiliano ya kisiasa, hivyo kuweza kuwa mazungumzo yenye  matunda chanya kati ya imani na hoja.  Papa anaonya juu ya mambo ya kidunia na ubabe kwamba yote mawili hubinya uhuru wa mtu katika kujieleza na hivyo kufanya  mazungumzo  kuwa magumu.

Mpendwa msikilizaji , katika kuzingatia kwamba,  hakuna binadamu anayeweza kuishi peke yake kama kisiwa, maana ni maumbile asilia ya binadamu,  kuishi na wengine, basi kila mmoja anaalikwa kuzingatia hili. Mungu alipomuumba mwanamme aliona haifai kuwa peke yake , akamuumba mwanamke ili wawe pamoja. Hivyo maisha ya binadamu ni mfumo wa maisha ya kutegemeana mmoja kwa mwingine, lakini kila mmoja kwa uhuru wake kamili.  Ndiyo maana uwepo wa mtu mwingine karibu nasi tunauhitaji.  Tunahitaji  kulipokea hili kwa uhuru kamili na kuheshimiana.

Tunapozungumzia uhuru huu , Dunia Mama anatoa ombi kwa wale wanaopenda kudhulumu uhuru wa wengine, pengine kutokana na mamalaka waliyopewa kijamii ,  na hasa tunawageukia  wale wanaopenda kujitukuza  na kufanya unyanyasaji au  kugandamiza   haki na uhuru wa wanafamilia eti kwa sababu tu  katika mpangilio wa maisha ya binadamu, wametajwa kuwa  kuwa kiongozi mkuu wa familia. Lakini kumbe, amri ya Muumba inasema , aliyekichwa cha familia anapaswa kuwa mtumishi mkuu wa familia.  Mtume Paulo aliandika,  “ kwa  vyovyote vile kila mmoja wenu na aishi kufuatana na vipaji alivyogawiwa na Bwana. Maana aliyeitwa na  Bwana akiwa mtumwa huyo huwa mtu huru kwa Bwana,  hali kadhalika aliyeitwa akiwa huru , huwa mtumwa wa Kristo( tazama 1Kor 7) Nyote mmenunuliwa kwa bei ya damu ili msiwe tena watumwa.

 Mpendwa,  Dunia Mama  anahoji na kukuomba utafakari kwa kina, kwa nini unawanyanyasa na kuwanyima  raha wanafamilia wako kwa kuwekea masharti makali makali ya kufuatwa,  na kupafanya nyumbani kama nyumba ya mahabusu au gereza?  Je bado wamnyima uhuru wa kujieleza mkeo  kwa kisingizio cha mila na desturi za kizamani? Mbona wafanya madhulumu ya kuwanyima uhuru wenzako  katika mazungumzo, wataka wewe peke yako usikilizwe na si wao . U wapi uhuru wao kimaisha?  Je watambua kuwa wao wanazijua haki na maana ya uhuru wao kuliko hata wewe?  Watu wenye hekina wanatambua kuwa huru haina maana ya kutenda kama wanavyotaka bila kujiheshimu au kuheshimu wengine. Wanajua kuwa uhuru kamili , ina maana ya kukataa madhulumu na uonevu, lakini si kukataa katika njia za ugomvi na matusi lakini kwa  unyenyekevu kuelimishana na kuvumiliana . Wanajua mwenye kuishi kwa uhuru kamili maana yake ni kuheshimu wengine .

Dunia Mama wiki hii, anatualika sote, kama wana familia, tuwezeshe  familia zetu  kuwa  chemchemi  ya  fadhila na huruma ili watu wote duniani waishi kwa uhuru kamili, katika kuzungumza, kutenda na hata kwenda anakotaka ili mradi hawabugudhi wengine.  

Makala haya hundaliwa nami TJ Mhella. Redio Vatican 








All the contents on this site are copyrighted ©.