2015-04-25 15:21:00

Uchaguzi mkuu nchini Burundi 2015: Hofu na wasi wasi vyatanda!


Padre Anaclet Mwumvaneza, Katibu mkuu wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Rwanda, Caritas Rwanda anasema kwamba, kutokana na wasi wasi wa machafuko ya kisiasa nchini Burundi, hadi sasa kuna wakimbizi elfu nane wanaohudumiwa na Caritas Rwanda. Kumekuwepo na muaji ya kinyama yanaofanywa na vijana nchini Burundi dhidi ya vyama vya upinzani. Hali hii imepelekea wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Burundi, wengi wao wa kiwa ni watoto wadogo wakiwa wameandama na mama zao.

Kwa sasa wakimbizi hawa wanahudumiwa kwenye kambi mbili kubwa zilizoanzishwa na Umoja wa Mataifa huko Buguser na Nyanza. Wahamiaji hawa anasema Padre Mwumvaneza wanahitaji msaada wa dharura, ili kuwawezesha kukabiliana na adha ya maisha kwa wakati huu. Hali ya kisiasa nchini Burundi kwa sasa ni tete kutokana na kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo tarehe 26 Juni 2015.

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi lilipinga wazo la kubadilisha Katiba ya nchi ili kutoka mwanya kwa Rais Pierre Nkurunziza kuwania tena madaraka kwa kipindi cha awamu ya tatu, jambo ambalo ni uvunjaji wa makusudi wa Katiba ambayo ni sheria mama. Maaskofu wanawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushinda kishawishi kinachotaka kuwagawa na kuwasambaratisha wananchi wa Burundi; mambo ambayo yanaweza kusababisha tena kinzani za kijamii na hatimaye, vita.

Katiba ya nchi inabainisha kwamba, baada ya vipindi viwili vya kuongoza nchi, kiongozi atatakiwa kuachia ngazi, ili mwananchi mwingine aweze kushika madaraka. Huu ni uamuzi wa busara unaopaswa kutekelezwa badala ya kupindishwa kwa ajili ya masilahi ya watu wachache kisiasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.