2015-04-25 12:10:00

Tanzania kuboresha Miundombinu yake ili kuongeza kasi ya Uwekezaji


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Mhe. Mhandisi Christopher Chiza (Mb) amewaeleza wananchi wa Visiwa vya Comoro pamoja na wafanyabiashara kuwa Serikali ya Tanzania imejithatiti katika kuboresha wigo mpana katika masuala ya ili kuweza kukuza uchumi na uwekezaji nchini. Amesema hayo akiwa anatoa Hotuba yake kwa Wadau na Wafanyabiashara kutoka Tanzania baada ya ufunguzi wa Komango la Biashara kati ya Comoro na Tanzania jana Alhamisi tarehe 23 Aprili, 2015.

“Miongoni mwa maeneo ambayo Serikali ya Tanzania imeweza kuyaboresha ili kurahisisha na kuongeza uwekezaji ni pamoja kujenga Miundombinu bora yaani  Barabara, kuboresha Viwanja vya Ndege, Bandari itarahishisha uchukuzi na kuongeza  fursa katika nchi SADC”, alisema Waziri Chiza. Chiza aliongeza kuwa, mazingira ya kibishara kwa Tanzania yanalindwa na Sera zilizopo kwa kupitia Sera ya Ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi yaani (PPP) inalinda na kusimamia masuala ya uwekezaji baina Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

Wafanyabiashara kutoka nchini Tanzania wametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na pamoja na ushuru wa forodha kuwa mkubwa visiwani Comoro, Usafiri usio wa uhakika unaosababisha bidhaa zao kuharibika mara kwa mara pamoja na mahitaji ya viza kuingia na kutoka nchi Comoro.

Mapema wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo Rais wa Visiwa vya Comoro Ikililou Dhoinine amesema, “tayari ameagiza Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi yake ishirikiane na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania kwa lengo la kuondoa matumizi ya viza baina ya Tanzania na Comoro ili kuweza kurahisha masuala ya biashara katika nchi hizi.

Waziri Chiza alimalizia kwa kusema kuwa, Visiwa vya Comoro vina fursa nyingi za uwekezaji na biashara ikiwemo huduma ya usafiri wa majini, anga pwani zenye madhari kwa uwekezaji wa Hoteli za kimataifa, ambapo amewashauri wawekezaji wa Tanzania kutumia fursa ya mkutano huo kuyabaini na kuyafanyia kazi.

Imetolewa na Francisca Swai

Afisa Habari

Ofisi ya Waziri Mkuu,

24 Aprili,2015








All the contents on this site are copyrighted ©.