2015-04-25 14:33:00

Siku ya kuombea miito duniani: Wakristo msilale, amasisheni miito!


Wakatoliki hawana budi kutambua dhamana na wajibu wao wa kulea na kukuza miito mitakatifu, ili Kanisa liweze kupata mihimili makini ya Uinjilishaji, inayojikita katika utakatifu wa maisha, ukweli, uwazi, lakini zaidi katika ushuhuda unaonesha imani tendaji. Hii ni changamoto ambayo inatolewa na Kardinali Manuel Clemente, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno katika maadhimisho ya Juma la kuhamasisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa, ambalo linahitimishwa katika Jumapili ya Yesu Kristo mchungaji mwema, Jumapili ya kuombea miito mitakatifu.

Kardinali Clemente anasema, wito ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Wakristo; na linapaswa kuvaliwa njuga na waamini wote na wala si na kikundi cha watu wachache ndani ya Kanisa. Miito inaendelea kupungua ndani ya Kanisa kwa vile waamini wanalala usingizi, badala ya kuchakarika kupandikiza, kukuza na kupalilia miito, ili kweli Kanisa liweze kupata “majembe ya nguvu” katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Wito si suala la maamuzi binafsi, bali ni sehemu ya mchakato wa kuitikia wito kutoka kwa Mungu mwenyewe, anayewataka waamini kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Wakristo kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, wawasaidie vijana kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu inayowachangamsha kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani. Kutokana na umuhimu wa miito mitakatifu kwa ajili ya maisha na utume, waamini hawana budi kujenga utamaduni wa kusali mara kwa mara ili kuombea miito, wasali kumwomba Bwana wa mavuno ili aweze kupeleka watenda kazi katika shamba lake; watenda kazi, wema, watakatifu na wachapakazi; watu ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa: kiroho na kimwili.

Kardinali Manuel Clemente, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno anawashukuru na kuwaombea wale wote ambao kwa njia moja au nyingine wamekuwa ni wadau wakuu katika kuhamasisha, kukuza na kudumisha miito mitakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, ili waendelee kutekeleza dhamana hii nyeti. Hawa ni watu ambao wanakumbana na mawimbi mazito, kwani leo hii licha ya umuhimu wa maisha na wito wa: Kipadre, Kitawa na Ndoa, kuna vijana wachache ambao wanathubutu kuacha yote na kuamua kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.