2015-04-25 11:53:00

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu sana kwa mafao ya wengi


Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anapenda kukazia kwa namna ya pekee majadiliano kati ya watu kama njia muafaka ya kutafuta na kuenzi mafao ya wengi. Huu ni mchakato unaowahamasisha watu kukutana katika ukweli na uwazi; urafiki na udugu, ili kubomoa kuta za utengano na kinzani zinazodumishwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kila mtu anapaswa kulinda na kudumisha utambulisho wake sanjari na ujenzi wa umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa.

Hii ni sehemu ya mhadhara uliotolewa na Kardinali Pietro Parolin kwenye Kitivo cha Taalimungu, Chuo kikuu cha Triveneto, kilichoko Kaskazini mwa Italia, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wasomi, inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama “Dies academicus”. Majadiliano si dhana ambayo inaelea kwenye ombwe au utaratibu wa kushirikishana mawazo, bali ni ukweli wa mambo na mwanzo mahusiano ya kweli yanayopania maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hapa anakumbusha kwamba, dhana ya mshikamano ni muhimu sana katika ujenzi wa haki na mafao ya wengi, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu badala ya kuendekeza utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita inayotaka kukidhi masilahi ya watu wachache ndani ya jamii, watu wenye uchu wa mali na madaraka. Mshikamano wa kimataifa unapania kwa namna ya pekee kukuza na kuendeleza fursa za kiuchumi na kijamii. Hapa kuna haja ya kusitisha vita na kuanza mchakato wa amani katika ulimwengu wa utandawazi na kwamba, mshikamano na upendo ni chanda na pete kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kanisa linapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani na kwamba, hii ni sehemu muhimu sana ya sera za mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Majadiliano ni njia pekee inayotumiwa na Vatican kuweza kukutana na mataifa yenye nguvu na uwezo wa kiuchumi na kijeshi. Kwa njia ya majadiliano, hapa misimamo mikali ya kitamaduni, kidini na hata pengine kitaalimungu inaweza kutoweka na watu kuanza kujikita katika ujenzi wa amani.

Kadiri ya mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, utamaduni wa majadiliano unapania kujenga madaraja ya watu kukutana katika ukweli na uwazi, ili kubomoa kuta za utengano na hali ya kudhaniana vibaya, inayopelekea vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Hali inavyojionesha kwa sasa kutokana na kinzani nyingi, inaweza kuonekana kana kwamba, majadiliano ni dhana ambayo haiwezekani kamwe! Kama ni kweli, basi, damu ya watu wasiokuwa na hatia itaendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia.

Lakini, ikumbukwe kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi, yanapania mafao ya wengi, kulinda na kudumisha maisha, utu na heshima ya binadamu; usalama na maridhiano kati ya watu wa rangi, kabila na dini mbali mbali; kwani uhuru wa kuabudu ni sehemu msingi ya haki za binadamu. Hapa Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na uhuru wa kuabudu.

Vijana wanaosoma kwenye vyuo vikuu hususan Barani Ulaya wahakikishe kwamba wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ya maisha kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kanuni maadili; mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kukosekana kwa vijana wengi ambao wanamezwa na malimwengu; utupu wa maisha ya kiroho ni chanzo cha vijana wengi kukimbilia katika uvunjaji wa sheria pamoja na kujiunga na makundi ya kigaidi. Huu ni mwanzo wa vijana kuwa na misimamo mikali ya imani na maisha!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema kwamba, inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya Serikali zinazotaka kuhalalisha kifo laini kisheria, jambo linalokumbatia utamaduni wa kifo kwa kushindwa kuheshimu zawadi ya maisha. Hili ni suala la kimaadili ambalo linapaswa kushughulikiwa kikamilifu, kwani hizi ni dalili za utupu na ukosefu wa matumaini kwa mambo msingi. Watu wajifunze kujenga na kuimarisha mahusiano, upendo, mshikamano badala ya kufungwa katika utamaduni wa kifo na hali ya kukata tamaa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.