2015-04-25 09:53:00

Jengeni mshikamano wa upendo unaorutubishwa kwa sala na Neno la Mungu


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 25 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Yohane Paulo II, ambao wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma ya Uinjilishaji inayotekelezwa na Mama Kanisa, utume ambao ulivaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Kutangazwa kwake kuwa Mtakatifu kumewawezesha wajumbe wa Mfuko huu kupata ari na mwamko mpya, ili kurithisha amana iliyoachwa na Papa Yohane Paulo II katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kusonga mbele zaidi katika historia ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anawashukuru wajumbe hawa kutokana na mchango wao katika sekta ya elimu miongoni mwa vijana. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwapenda na kuwathamini sana vijana; akaonesha kipaumbele cha pekee katika utume wao. Mfuko wa Yohane Paulo II unapania kuendeleza karama na ubaba wake, ili viweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Baba Mtakatifu anawapongeza Wakleri na Waamini walei wanaosaidia majiundo makini ya vijana, watambue kwamba, wanatoa mchango mkubwa kwa vijana ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha na shughuli za kichungaji katika ulimwengu mamboleo. Wajumbe hawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kujichotea utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa na kwa namna ya pekee katika mshikamano, neno ambalo linaonesha nguvu ya kinabii.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa Mfuko wa Yohane Paulo II kuhakikisha kwamba, wanamwilisha dhana ya mshikamano katika maisha na utume wao; huku wakiendelea kujikita katika umoja na udugu wa Kikristo unaorutubishwa kwa njia ya sala na wanyenyekevu kwa Neno la Mungu. Baba Mtakatifu amewakabidhi wajumbe hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama ambaye, Mtakatifu Yohane Paulo II aliyakabidhi maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.