2015-04-24 16:24:00

Ukikutana na Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha, lazima ugeuke!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kichoko mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 24 Aprili 2015 amesema kwamba, mwamini anayekutana na Yesu kwa mara ya kwanza, anapata mageuzi na kuanza mwelekeo mpya wa maisha, changamoto kwa Wakristo kufanya kumbu kumbu hii katika maisha yao. Yesu alipokutana na Saul kwa mara ya kwanza alipokuwa njiani kwenda kufanya madhulumu dhidi ya Wakristo, aliyebadililika na kuwa Mtume na Mwalimu wa Mataifa, Saulo, mtesaji, akapewa jina jipya, Paulo ambaye amewawezesha waamini wengi kukutana na Yesu kwa njia ya Maandiko Matakatifu.

Yesu alipokutana na Yohane na Andrea, wakaacha yote na kuamua kumfuata katika safari ya maisha yake yote, Simone, akapewa jina jipya kuwa Petro na juu ya mwamba huu, Yesu amejenga Kanisa lake. Yesu alipokutana na yule Mwanamke Msamaria, maisha yake yakabalika na kuwa mtu mwema zaidi na shuhuda wa matendo makuu ya Mungu katika maisha yake. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Mkoma, mwenye shukrani alipokutana na Yesu akagundua kwamba, ameponywa ugonjwa wake, akarudi kumshukuru na kumtolea Mungu sifa na utukufu. Bila shaka wengi wanakumbuka yule mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa miaka mingi, alipogusa pindo la vazi la Yesu, akaponywa msiba wake.

Baba Mtakatifu anasema haya ni matukio ambayo yanaacha kumbu kumbu ya kudumu kwa waamini wanapokutana kwa imani na matumaini na Yesu, kwa hakika anawaletea mabadiliko na mageuzi katika maisha. Ni rahisi sana kwa Wakristo kusahau matukio haya, lakini Yesu anayakumbuka, jambo la msingi ni kufanya tafakari ya kina ili kuangalia lini na wapi wameweza kusikia uwepo wa Kristo katika shida na mahangaiko yao, katika raha na karaha kwani imani ya Kikristo ni mchakato wa kukutana na Yesu, kama Saulo alivyokutana na Yesu, akabadilika na kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa.

Waamini wajiulize kutoka katika undani wa maisha yao, lini ambapo wameweza kusikiliza kwa umakini mkubwa Yesu akizungumza nao na kuwaletea mabadiliko ya kweli! Yesu anaendelea kukuza na kudumisha upendo na kila mwamini katika maisha yake.

Na Padre richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.