2015-04-24 16:36:00

Mauaji dhidi ya Wakristo ni ukiukwaji wa uhuru wa kuabudu na haki zao!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia lina laani mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya Wakristo kutoka Ethiopia hivi karibuni nchini Lybia. Maaskofu wanasema, Wakristo waliokuwa huko Lybia hawakuwa ni wanasiasa, askari wa kukodishwa wala watu hatari kwa usalama na maisha ya watu, bali ni vijana wahamiaji waliokuwa na matumaini ya kuleta mabadiliko katika maisha yao na familia zao sanjari na kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi yao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia linasikitishwa sana na mauaji haya ya kinyama na kwamba, Wakristo hao wameyamimina maisha yao kwa sababu walisimama kidete kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Uhuru wa kuabudu ni haki msingi ya binadamu inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote bila ubaguzi wa rangi, kabila au mahali anapotoka mtu.

Maaskofu wanasema, wanaofanya vitendo hivi vya kigaidi kamwe hawawezi kuhalalisha kwamba, wanafanya hivyo kwa misingi ya kidini, kwani vitendo hivi vinakwenda kinyume kabisa cha imani kwa Mwe nyezi Mungu, ambaye hata watu wengine wanamwabudu. Haiwezekani kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia kwa misingi ya kidini na kwamba, dini kubwa duniani zimeenezwa kwa njia ya wahamiaji na wakimbizi na kwamba, hata Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, iliweza kufika Barani Afrika kama wakimbizi, ikapewa hifadhi. Huu ndio ukarimu ambao Bara la Afrika linapenda kuonesha hata nyakati hizi, kwa kutoa hifadhi ya wakimbizi na wahamiaji pasi na ubaguzi wowote, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki linasema kwamba, wahamiaji na wakimbizi kutoka Ethiopia waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kadiri ya sheria za kimataifa sanjari na kuhakikisha kwamba, usalama wa maisha yao unalindwa pia. Maaskofu wanataka wale wote wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu kuacha mara moja mchezo huu mchafu unaowadanganya vijana kukimbia nchi yao kwa ahadi za uwongo.

Vijana nao wanatakiwa kuwa makini kuhakikisha kwamba, wanapata nyaraka muhimu kabla ya kuanza safari ughaibuni ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama na maisha yao. Jambo la kwanza ni vijana kutoa kipaumbele cha kwa kuonesha uzalendo na utashi wa kufanya kazi nchini mwao, kwani huko wanakodhani kwamba, kuna “asali na maziwa” mambo ni kinyume kabisa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia linahitimisha masikitiko yake kwa kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo waliouwawa kinyama huko Lybia. Wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa mshikamano na upendo wa kidugu aliouonesha kwa ujumbe aliomwandikia Patriaki Abuna Matthias wa Kanisa la Kiorthodox la Ethiopia. Damu ya Wakristo inayoendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia ni ushuhuda wa kilio kinachopaswa kusikilizwa na watu wale ambao wamekabidhiwa dhamana ya ulinzi na usalama wa raia wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.