2015-04-24 16:13:00

Kanisa nchini Namibia na Lesotho, litoe kipaumbele kwa maskini!


Namibia na Lesotho ni nchi ambazo imani ya Kikristo inaendelea kuchanua kama Mwerezi wa Lebanon, kazi na matunda ya jasho la Wamissionari waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa; dhamana ambayo imeendelezwa na wazalendo walioingia na kufanya kazi katika shamba la Bwana. Hizi ni nchi ambazo zinakabiliwa na changamoto katika medani mbali mbali za maisha, lakini Mwenyezi Mungu anaendelea kuzilinda na kuzitunza kwa maji ya neema yake.

Namibia na Lesotho ni nchi ambazo Kanisa limewekeza sana katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya kijamii, kazi inayotekelezwa kwa moyo wa upendo na ukarimu; changamoto ya kuendeleza baraka zinazojitokeza katika utume huu, ili kuzaa matunda yanayokusudiwa. Hii ni sehemu ya hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Namibia na Lesotho, alipokutana na kuzungumza nao mjini Vatican, siku ya Ijumaa, tarehe 24 Aprili 2015 wakati wa hija yao ya kitume, inayofanyika mjini Vatican, walau kila baada ya miaka mitano.

Baba Mtakatifu anasema, ubinafsi, rushwa na ufisadi wa mali ya umma sanjari na athari za ugonjwa wa Ukimwi ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Mambo haya yanahitaji kwa namna ya pekee, majiundo makini katika fadhila za Kikristo ili kuchuchumilia utakatifu wa maisha na kwa njia ya ushuhuda wa maisha amini na matakatifu yanayotolewa na Maaskofu pamoja na Mapadre, ambao ni wasaidizi wao wa kwanza katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wanapaswa kuwa karibu zaidi na Mapadre wao, ili waweze kujifungamanisha na Kristo, tayari kuchangia katika mchakato wa mageuzi yanayolenga kuipyaisha Jamii ya Kiafrika.

Baba Mtakatifu anasema, kuna familia nyingi ambazo zinateseka kutokana na wanandoa kutengana kwa sababu ya kazi mbali na miji yao au kwa kutalakiana; wote hawa wanahitaji kusaidiwa na Kanisa katika safari ya maisha; kwa kujikita katika majiundo makini ya maisha ya ndoa na familia mintarafu Sakramenti ya Ndoa Takatifu pamoja na kuwasaidia wanandoa kuendelea kushiriki kikamilifu katika Sakramenti ya Upatanisho, kwa kuhakikisha kwamba, Mapadre wapo tayari kuwahudumia waamini wao.

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza Maaskofu kutoka Namibia na Lesotho kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi na tunu bora za maisha ya ndoa na familia dhidi ya mmong’onyoko wa kanuni maadili na mwelekeo tenge kuhusu dhana ya ndoa na familia. Ikumbukwe kwamba, familia ni chemchemi ya amani ni mahali muafaka pa mtu kujifunza na kumwilisha katika maisha yake dhana ya msamaha, amani na upatanisho.

Familia ni chimbuko la miito mitakatifu ya upadre na utawa, tayari kuwashirikisha wengine, upendo ambao wameuonja kutoka kwa wazazi wao ndani ya familia. Watoto wanaotoka katika familia za namna hii wako tayari kujisadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Kanisa. Wakati huu ambapo kuna upungufu mkubwa wa miito ya kipadre na kitawa kuna haja ya kushuhudia ukweli na furaha inayojikita katika uaminifu wa maisha ya Kipadre na kitawa yanayofumbatwa katika mashauri ya Kiinjili, yaani: Utii, Ufukara na Useja. Kwa njia ya ushuhuda huu, kwa hakika anasema Baba Mtakatifu, miito ya kipadre na kitawa itaweza kuchanua na kushamiri ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu wenzake kuendelea kujikita katika maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu; kwa kuwaongoza na kuwasimamia Mapadre wao barabara pamoja na kuhakikisha kwamba, wanapata majiundo endelevu ili waweze kutekeleza vyema utume wao. Baba Mtakatifu anawaomba Maaskofu wa Namibia na Lesotho kuwafikishia Wakleri wao salam na matashi mema kutoka kwake.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanaibua mpango mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya kuhudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Pale ambapo Kanisa linamezwa na malimwengu, hapo hakuna nafasi kwa maskini. Kwa kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, Maaskofu wanaweza kuwa ni msaada mkubwa kwa Familia ya Mungu wanayoihudumia, kuiongoza na kuitakatifuza. Anawataka waendelee kuonesha ushuhuda wa huduma kwa Familia sanjari na kuimarisha vyama vya kitume, ili viweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa: kiroho na kimwili, kwani mchango wao ni muhimu sana.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuwa ni watu wa sala, kama alivyokuwa Mwenyeheri Joseph Gerard, aliyekuwa msikivu kwa Roho Mtakatifu katika maisha yake na kwamba, sala ni muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji, chemchemi ya furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, hija ya kitume inayofanywa na Maaskofu itawakirimia huruma ya Kristo inayopanya, ili kuzaa matunda kwa wale wote wanaowaongoza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.