2015-04-23 09:08:00

Ya leo ni kali! Ameamua kujifagilia mwenyewe!


Jamani eti raha jipe mwenyewe! Leo Yesu anaamua kwa macho makavu kabisa kujifagilia mwenyewe kuwa ni mchungaji mwema! Binadamu wote kuanzia watoto hadi wakubwa tunavutika na mambo mazuri kama vile muziki. Mtoto akilia anabembelezwa na mama kwa kuimbiwa wimbo hadi mtoto analala usingizi. Binadamu tunastaajabishwa na kazi ya ufundi, ushairi, uchoraji, tamthlia, na kazi mbalimbali za sanaa kwa vitu vizuri vinavyopendeza. Kustaajabia ni kutafakari. Wanasanii kama vile, wanamuziki, mafundi mbalimbali, waandishi wa mashairi, wa tamthlia, wachoraji nk ni watu wanaotafakari uzuri katika fani yao kisha huitafsiri katika lugha inayoonekana hadi kuwavuta na kuwastaajabisha wengine. 

Picha nyingine inayoweza kueleza maana ya uzuri tunaiona katika kazi ya uumbaji, mathalani tunaposifia  mti mzuri kwa vile unatoa matunda matamu, tunasema mwembe mzuri, mchungwa mzuri, mpapai mzuri, mbegu nzuri, maua mazuri nk. Yesu anapompamba mwanamke aliyempaka mafuta alisema: “mwanamke ametenda jambo zuri,” Kadhalika katika uongozi wowote ule utawasikia watu wanampamba kwa sifa wakisema, “Tunaye kiongozi mzuri.”

Jumapili ya nne ya Pasaka ni ya Yesu Mchungaji Mwema. Lakini Injili ya Yohane haimtaji Yesu kuwa mchungaji mwema kama tusomavyo katika tafsiri ya kiswahili “Mimi ndimi mchungaji mwema.” Neno la kigiriki Kalos lililofasiriwa kama “wema” ni kalos maana yake ni nzuri, au safi, mwenye kupendeza au mwenye kumeremeta, mwenye thamani, azizi, wa kufaa, wa kustaajabia. Kwa hiyo neno Kalos halina uhusiano na wema wenye maana ya maadili. Kwa hiyo ufasiri mwafaka ungekuwa “Mimi ndimi mchungaji mzuri.”

Yesu anajinadisha na kujifagilia mwenyewe na anatoa vigezo vinavyomstahilisha kuwa na sifa ya jina hilo. Kwa hiyo leo tunaalikwa kuustaajabia au kutafakari uzuri wa mchungaji. Yesu anaanza kujitambulisha mwenyewe kama alivyojitambulisha Mungu katika Agano la Kale kitabu cha Kutoka alipotamka jina lake kuwa. “Mimi ndimi.” Kadhalika Yesu anatangaza jina lake kuongeza sifa kwamba, “Mimi Ndimi Mchungaji Mzuri.” Kigezo cha kwanza kinachomfanya Yesu kuwa mchungaji mzuri ni hiki kwamba “Mchungaji mzuri huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.”

Mchungaji mzuri hajionei huruma bali anatoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake yaani kwa wale anaowapenda. Yesu anafikiria furaha ya wenye shida. Mchungaji aina hiyo ni tofauti na mfanyakazi wa mshahara. Hapa tunakumbana pia na wale wanaojifanya kuwa marafiki wa Mungu wakitegemea kupata kitu kinachowapendeza. Hayo ni maisha ya kinafiki na ya mfanyakazi anayetaka kumfaidi Mungu. Kristu ametoa maisha yake bure kutokana na upendo alio nao kwetu. Kuwa mfuasi mzuri wa Yesu maana yake kutoa uhai wetu bure kwa ajili ya upendo na kwa ajili ya kumfanya mwingine kuwa na furaha.

Mfanyakazi wa mshahara afikapo mbwamwitu kuvamia kundi la kondoo, atakimbia na kuacha kondoo waliwe. Mbwamwitu ni jina linalomaanisha adui wa kondoo. Kila wakati na katika kila jamii kuna mbwamwitu wake. Tunao mbwamwitu wa kondoo ambao mchungaji mzuri analikingia kifua kundi lake dhidi ya mbwamwitu wanaoingiza roho ya uadui, roho ya maadili mabovu yasiyotofautisha jema na baya. Mbwamwitu hutuzuia kuona watu wema wanaoweza kutuonesha maadili mema. Mchungaji mzuri anatulinda dhidi ya wachungaji wanaojidai kuwa ni wema kumbe ni wabaya. Aina hiyo ya mbwamwitu wanaweza kuwapo pia katika makundi ya kikristu. Yatubidikuwa macho na wenye roho hii ya mbwamwitu au ya watu wasio na nia njema.

Kigezo cha pili ni maelezo zaidi ya “Mchungaji mzuri huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.” yaani ni mchungaji yule anayemfanya kondoo awe mzuri. Ni mchungaji yule anayempenda kondoo kwa ajili ya kondoo. Kunaweza kutokea wengine wanatupenda lakini wanakuwa na lengo la binafsi yaani kwa maslahi yao binafsi kwa vile “Mkono mtupu haulambwi.” Hatuna budi kujiuliza kwa sababu gani na kwa namna gani tunampenda mwingine. Kristu anatupenda kwa sababu anatupenda kiasi cha kutoa uhai wake kwa ajili ya upendo yaani anatupenda tu ili tuwe na furaha.

Kigezo cha tatu, “Mimi ni mchungaji mzuri; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.” Kujua huku kunamaanisha mahusiano ya umwandani kati ya mchungaji na kondoo. Kama vile kukutana kwa wenye kutakiana mema, yaani kule kutajirishana, kutendeana mema, kufikiriana mema. Kufahamiana, kujuana, kuungana. Kigezo cha nne Yesu anasema, “Nami hutoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo” yaani kutolea maisha kwa anaowapenda.

Kigezo cha tano ni upendo kwa wote. “Na Kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta.” Hapa hamaanishi kuwaingiza kondoo katika kizizi kimoja, la hasha, kwani aya za mwanzo za sura hii zinasema: “Mimi ni mlango; na mtu akiingia kwa mimi, ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Yesu anafungua mlango wa kizizi ili kondoo watoke kizizni wawe huru kwenda malishoni. Kondoo hao wamefungiwa katika mazizi na wakuu au na wale wanaowakandamiza kwa hoja za kidini au kisiasa. Kwa hiyo yaonekana kuna vizizi vingi vinavyowafungia watu ndani na Yesu anataka kuwafungulia watoke nje. Mathalani kuna mazizi yanayomfungia mwanamke ndani ya nyumba kama mtumwa, kuna wafanyakazi wanaokandamizwa na mabwana wao wa kazi, hawa yabidi wafunguliwe ili wapate uhuru wao. Mchungaji mzuri anawafungulia watu wote kutoka katika vizizi vya kitumwa kama hivyo. Mchungaji wa namna hiyo ni mzuri na anaweza kupendwa na ni uzuri anaouhitaji kila mtu hapa duniani. Kiongozi mzuri anavutia mtu yeyote yule.

Kisha Yesu anasema: “Na sauti yangu wataisikia,” kwamba katika imani hakuna kulazimishana budi kila mmoja afuate imani kwa uhuru wake na kwa upendo wa dhati. Ahadi anayoitoa Yesu kwa watakaosikia sauti yake na kuifuata ni kwamba “hatimaye kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.” Fasuli hii nayo budi ieleweke vizuri. Yesu hajafika kuwafungua watu kutoka kizizi kimoja na kuwafungia katika kizizi chake na yeye ndiye awe mchungaji wake, la hasha, bali yasema hatimaye kutakuwa na kundi mmoja na mchungaji mmoja. Yesu anatumaini kwamba kutakuja siku ambapo makundi hayo yatafuata mapendekezo mazuri ya mchungaji mzuri, na makundi hayo yatakuwa na fikra ya mchungaji mzuri, na yataakisi uwepo wa mchungaji mzuri hapa ulimwenguni yaani kutakuwa jamii moja nzuri itakayofuata mapendekezo ya mchungaji mmoja aliye mzuri yaani Yesu wa Nazareti.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.