2015-04-23 08:50:00

Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema!


Tunaendelea kuumega mkate Neno la Mungu Dominika ya IV ya Pasaka, Dominika ambayo Mama Kanisa ameiweka rasmi kuwa Dominika ya Mchungaji Mwema. Ujumbe toka Neno la Mungu katika Dominika hii ni Bwana ndiye mchungaji mwema. Ujumbe huu tunaupata katika somo la Injili ya Yohane sura ya kumi. Ni katika mantiki hiyo Mama Kanisa ameiteua Dominika hii kwa ajili ya kuombea miito katika Kanisa. Twakumbuka kuwa mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache, kumbe tumwombe Bwana wa mavuno apeleke miito mitakatifu ili taifa lake lipate zawadi ambazo Kristu atoa kwa njia yao.

Vijana mnaalikwa kuwa mashujaa wa kusikia sauti ya Mungu inayowaita daima. Nasi tuliokwishaitika twaalikwa na Mama Kanisa kuwasidia wengine ili wasikie sauti ya Mchungaji Mwema.

Katika somo la kwanza tunaona Mitume wakiendelea kwa kasi na nguvu kubwa kutangaza ujumbe wa ufufuko wakipata nguvu katika Kristu Mchungaji mwema. Wanapohubiri na kufanya uchungaji wao wanaponya wagonjwa, na sifa hii ya uponyaji wanampa Bwana. Wanasema mbele ya Wayahudi, yule mliyemwua amefufuka na ndiye aponyaye, amefanywa kuwa jiwe kuu la pembeni ingawa mlilikataa! Wanaendelea kusema kuwa tubuni kwa maana hakuna wokovu isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristu Masiha mwana wa Mungu aliyemfufuka. Mpendwa unayenisikilza mwaliko huu ni kwako na hivi hakikisha unajiweka katika upande wa kukaa na Mchungaji mwema maana ndiye mwokozi pekee na taa kiongozi wa maisha yako.

Katika somo la pili Mtakatifu Yohane anayo furaha kuu, furaha ya Pasaka. Ni kwa njia ya furaha hii anatangaza pendo la Mungu kwa mwanadamu awaye yote, akisema kwa njia ya Yesu Kristu mfufuka tumekuwa wana wa Mungu, na ingawa hatujajua itakuwaje hapo mbele lakini tunauhakika yatakapokuwa yamekamilika tutafanana naye maana tutamwona alivyo.

Kama nilivyokwisha dokeza hapo katika utangulizi somo la Injili linatupa picha ya Mchungaji Mwema. Kristu ndiye mchungaji mwema kwa maana huwachunga kondoo, huwalinda na huwapeleka katika malisho ya majani mabichi. Sifa kubwa na ya juu ya mchungaji mwema ni ile ya kujitoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake. Kristu anajitoa kwa ajili ya ulimwengu, anamwaga Damu yake Takatifu sana inayotakasa ulimwengu, anakubali kuwekwa msalabani anakufa kifo cha aibu kwa ajili ya kuleta wokovu kwa mwanadamu. Hakika huu ni upendo upeo, upendo usiopimika!

Bwana anatualika katika ufuasi wetu kuwa wachungaji wema wa taifa lake na hivi kila mmoja wetu ajitahidi walau kutoa nguvu na jasho lake kwa ajili ya kutakatifuza ulimwengu. Akazanie maisha adili na umoja kamili na Mungu na hasa kwa njia ya toba. Wale walio wachungaji kwa njia ya Daraja takatifu wahakishe malisho ya sakramenti kwa waamini ndiyo shime yao. Wale walio wachungaji kwa njia ya familia wahakikishe familia inakua na kukomaa katika maisha ya fadhila dira akiwa ni Kristu Mchungaji Mwema. Ndiyo kusema nyanja zote za maisha ya kila siku zishike dira na kasi katika kulinda uhai na afya ya mwili na roho zikiongozwa na Kristu mchungaji mwema.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican ninakutakia heri na baraka za Mungu nikikuombea daima ili ushike wito wako wa kuwa mchungaji mwema katika taifa, familia ya Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.