2015-04-23 08:17:00

Siku ya 52 ya Kuombea Miito Duniani: Tokeni kumhudumia Mungu na jirani


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya nne ya kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo mchungaji mwema, yaani tarehe 26 Aprili 2015, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoka Daraja Takatifu la Upadre, kwa Mashemasi walioandaliwa. Hii itakuwa ni jumapili ya 52 kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, kwani mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Ni siku ambayo waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuombea miito, ili Kanisa liweze kuwapata wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa; watu makini, wema, watakatifu na wachapakazi, ambao daima wako tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Dhamana ya kimissionari na mchakato wa Uinjilishaji ndicho kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa. Anasema, wito wa Kikristo unajikita katika mang’amuzi ya mtu kutoka katika ubinafsi na undani wake, ili kumwendea Mwenyezi Mungu na kujisadaka kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko wa pekee kwa vijana kutokuwa na woga wa kutoka katika undani na ubinafsi wao, tayari kuanza mchakato wa hija, wakiyaelekeza macho yao kwa ajili ya maskini na watu wanaohitaji kusikia na kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kutoka ni mang’amuzi msingi katika wito, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 52 ya kuombea Miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Katika Kanisa ambalo kimsingi ni la kimissionari, wito unachipuka, unakua na kukomaa katika mazingira ya kitume, jambo linalowezekana, ikiwa kama mwamini anathubutu kutoka katika ubinafsi wake, kwa kufanya hija, kama ile iliyofanywa na Watu wa Mungu kama yanavyosimulia Maandiko Matakatifu kutoka Misri kuelekea kwenye nchi ahadi, iliyojaa maziwa na asali. Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kutoka katika utumwa wa ubinafsi ili kuambatana na kupata maisha mapya kwa Yesu Kristo. Hili ndilo Fumbo ambalo linafumbatwa katika historia ya wokovu na mwelekeo wa imani ya Kikristo.

Kutoka ni kiini cha kila wito wa Kikristo anasema Baba Mtakatifu Francisko, kwani hii ni changamoto ya kutoka katika anasa, ukavu wa maisha yanayojikita katika ubinafsi ili mwamini aweze kuyaelekeza maisha yake kwa Yesu Kristo. Ni kutoka kunakotambua utu wa mtu na kwamba wito wa Kikristo unafumbatwa katika upendo wenye mvuto unaovuka mipaka ya mtu binafsi na kuanza mchakato pevu na wa kudumu ili kutoka katika ubinafsi na kuelekea katika uhuru unaojikita katika sadaka ya mtu binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa siku ya 52 ya kuombea miito duniani anabainisha kwamba,  kutoka huku kunafumbata dhamana ya kimissionari na uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa; hili ni Kanisa linalotoka ili kwenda kukutana na Watoto wa Mungu, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, ili kuganga na kuponya madonda yao. Kanisa linaloinjilisha linahamasishwa kutoka ili kukutana na watu, kuwatangazia Habari Njema inayowaletea wokovu; kwa kuwaganga na kuwaponya watu: kiroho na kimwili kwa njia ya neema ya Mungu na kuwafariji maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wito wa Kikristo ni dhamana inayojikita katika huduma bora na makini kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani sanjari na kujikita katika mshikamano wa udugu na upendo, hususan kwa maskini na wahitaji zaidi.

Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee vijana wa kizazi kipya kutoogopa wala kukatishwa tamaa na wasi wasi kuhusiana na mambo ya mbeleni; yanayoweza kuzimisha ndoto yao kama “kibatari”. Anawataka vijana kutoogopa kutoka katika ubinafsi wao na kuanza hija ya kufuata nyayo za Yesu, kama alivyofanya Bikira Maria, mfano wa kila wito, ambaye kamwe hakusita kusema, Ndiyo, pale alipoitwa na Mungu, ili aweze kuwa Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Vijana wanakumbushwa kwamba, wito ni mchakato wa kutoka katika ubinafsi ili kumwendea Mwenyezi Mungu na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.