2015-04-23 14:50:00

Papa Francisko kutembelea Cuba! Mjumbe wa amani na upatanisho!


Familia ya Mungu nchini Cuba imepokea kwa mikono miwili taarifa za hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cuba wakati akiwa njiani kuelekea Marekani kuwa huu ni ujumbe wa matumaini na mwanzo mpya katika mchakato wa majadiliano yanayopania kukuza na kudumisha mafao ya wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba linapenda kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu na wasaidizi wake wa karibu katika mchakato wa majadiliano ya kidplomasia ulioiwezesha Cuba na Marekani kufungua ukurasa mpya wa mahusiano ya kidiplomasia, baada ya kutunishiana misuli kwa takribani miaka 50 iliyopita.

Monsinyo Josè Felix Garcia, Katibu mwambata wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi anayethubutu kutumia karama na mapaji yake kwa ajili ya mafao ya wengi; katika wema na uzuri; katika furaha na majonzi. Ni kiongozi anayethubutu bila woga kuonesha msimamo na kile ambacho kinaugusa undani wa moyo wake. Amethubutu kutembelea maeneo ambayo mtutu wa bunduki bado unarindima, ili kuwatangazia huko Injili ya amani, furaha na matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko ni Kiongozi anayejipambanua kwa kukazia majadiliano kati ya watu, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo, na udugu, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, shida, magumu na changamoto za maisha zinatatuliwa kwa njia ya majadiliano na wala si kwa mtutu wa bunduki! Ni mtu anayesimamia haki, amani, ustawi na mafao ya wengi, lakini kipaumbele ni kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa tatu kutembelea Cuba. Kwa mara ya kwanza Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Cuba kunako mwaka 1998; Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akatembelea Kisiwani humo kunako mwaka 2012 na sasa Papa Francisko, tayari anajiandaa kuitembelea Familia ya Mungu nchini Cuba.

Wakati huo huo, Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anaendelea na hija ya kichungaji nchini Cuba kwa mwaliko wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Stella amewahi kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Cuba katika kipindi cha mwaka 1993 hadi mwaka 1999.

Na padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.