2015-04-22 08:41:00

Utumwa mamboleo: Ni suala la kuvaliwa njuga kimataifa!


Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii baada ya kuhitimisha mkutano wake wa mwaka, inapendekeza uwepo wa Wakala wa Kimataifa atakayesimama kidete kupambana na utumwa mamboleo kimataifa baada ya Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutia sahihi katika protokali itakayokuwa imeanzishwa. Ni changamoto ambayo imetolewa tarehe 21 Aprili 2015 na Bibi Margaret Archer, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican.

Anasema, kuna haja ya kulivalia njuga tatizo la biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kwa kupambana na tatizo hili katika mizizi yake; yaani mambo yanayopelekea uwepo wa tatizo hili pamoja na kuwasaidia waathirika. Kwa maneno mengine, kuna haja ya kupambana kikamilifu na utumwa mamboleo, kazi za nguvu na suluba na biashara haramu ya viungo vya binadamu; mambo ambayo yanaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Wahamiaji na wageni wanahifadhiwa na nchi wahisani wanapaswa kuheshimiwa na kutunzwa kama binadamu, kuliko hali ilivyo kwa sasa katika nchi nyingi.

Waathirika wa utumwa mamboleo wanapaswa kusaidiwa kikamilifu wanaporudishwa makwao, ili waweze kuanza maisha kwa matumaini mapya, kuliko kuwatelekeza, hali ambayo inagumisha zaidi maisha yao, kwani wengi wao ni wale wanaotoka katika mazingira duni na maskini. Kanisa linapenda kuendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wanaosimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa kupambana na biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo.

Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 70% ya watu wanaotumbukizwa katika utumwa mamboleo ni wanawake na wasichana na kwamba, asilimia 72% ya wafanyabiashara haramu ya binadamu ni wanaume. Professa Stefano Zamagni anafafanua kwamba, kuna idadi kubwa ya wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika biashara ya ngono na kazi za suluba, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kupambana na magenge ya uhalifu kimataifa, jambo ambalo halijapewa msukumo wa kutosha.

Professa Zamagni anasema kwamba, ili kukabiliana na watu wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka ambao wanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa wahamiaji na wakimbizi kwenye Bahari ya Mediterrania, wataifishiwe vyombo vyao vya usafiri, ili kukomesha maafa ambayo kwa sasa hata hakuna tena mtu anayeomboleza, kwani huu ni wimbo usiokuwa na kiitikio! Ubinafsi na unyama uliokithiri ni mambo ambayo yanaendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Huu ni utandawazi usiojali mahangaiko ya wengine wala kujikita katika umoja, udugu na mshikamano. Faida kubwa ni chanzo kikuu cha majanga yanayomkabili mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Professa Pierpaolo Donati anasema kwamba, kuna haja ya kutenganisha wahamiaji haramu na watu ambao wanatumbukizwa katika utumwa mamboleo. Kuna haja ya kwa Jumuiya ya Kimataifa kupambana na utumwa mamboleo unaokumbatiwa pia na biashara ya ngono kwa wanawake na wasichana hasa kutoka katika nchi maskini zaidi duniani. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kubainisha bidhaa zinazozalishwa kutokana na kazi za suluba na kwamba, ili kupambana na biashara haramu ya binadamu, kuna haja ya watu kuhamasishwa kujitolea viungo vyao kama Wasamaria wema, ili kuokoa maisha ya watu badala ya kugeuza viungo kuwa ni biashara. Jamii ijenge na kudumisha utamaduni wa ushirikiano na mshikamano katika ngazi mbali mbali.

Kwa habari zaidi kuhusu biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaweza kutembelea mtandao wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kwa anuani ifuatayo: www.endslavery.va. Taasisi hii inataka kuwa msaada mkubwa kwa wadau mbali mbali wanaojifunga kibwebwe kupambana na utumwa mamboleo, unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu; dhamana ambayo Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 ameikabidhi Taasisi hii ya kipapa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.