2015-04-22 07:44:00

Scholas Occurentes, UNICEF: Mkataba wa maboresho ya elimu kwa vijana


Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF kwa kushirikina na Shirikisho la Mpira wa miguu Amerika ya Kusini Conmebol, kwa pamoja yameamua kuunganisha nguvu ili kusaidia mchakato wa utekelezaji wa malengo ya mtandao wa elimu unaojulikana kama “Scholas Occurentes” ulioasisiwa na Baba Mtakatifu Francisko. Mashirika haya kwa pamoja, siku ya Jumatatu, tarehe 21 Aprili 2015 mbele ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, yametiliana sahihi mkataba wa ushirikiano, tukio ambalo pia limehudhuriwa na viongozi wakuu wa UNICEF Bwana Anthony Lake; Wakurugenzi wakuu wa mtandao wa shule Enrique Palmeyro pamoja na Josè Maria del Corral. Askofu mkuu Marcelo Sànchez Sorondo, mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya elimu jamii amehudhuria pia.

Lengo kuu la mkataba huu ni kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi wanaoishi katika mazingira magumu kupata fursa, uelewa na nyenzo za kujifunzia katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia; sanaa na michezo; mambo msingi yatakawasaidia vijana kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii. Kwa kipindi cha miaka mitano UNICEF na Scholas watashirikiana kwa karibu zaidi katika kuendesha kampeni mbali mbali katika mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana wanaoishi katika mazingira magumu. Wadau hawa wanatarajiwa kubainisha mbinu mkakati utakaotumika ili kufanikisha malengo haya. Wanaangalia jinsi ya kutumia matukio makubwa ya kimataifa yanayowashirikisha vijana, ili kuendesha kampeni hii kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Mtandao wa elimu umewekeana pia mkataba na Shirikisho la Mpira wa miguu Amerika ya Kusini, Conmebol, ambalo litachangia kiasi cha dolla 10, 000 za Kimarekani kwa kila goli la adhabu litakalookolewa wakati wa mashindano ya Kombe la Amerika ya Kusini, litakalokuwa linatimua vumbi nchini Chile. Fedha hii itatumika kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maboresho ya elimu kwa nchi za Amerika ya Kusini zitakazokuwa zinashiriki. Mtandao wa shule kimataifa utaweza kufaidika moja kwa moja au kwa kutumia mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki au Mashirika mengine ya misaada yanayojipambanua kwa kukuza ushirikishwaji wa watu na ujenzi wa misingi ya haki na usawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.