2015-04-22 12:06:00

Mwaka wa Familia Jimbo kuu la Mwanza: Kazi na kusherehekea maisha!


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Familia, Jimbo kuu la Mwanza, Askofu mkuu Thaddeus Ruwa’ichi aliandika barua ya kichungaji kwa Familia ya Mungu jimboni humo akifafanua familia katika Maandiko Matakatifu; maudhui na hatimaye kazi na uwajibikaji, mada ambayo Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, itakayofanyika mwezi Oktoba hapa mjini Vatican. Barua ya kichungaji inagusa mambo msingi katika maisha na utume wa Familia, ili ziweze kutoka kifua mbele, tayari kutangaza Injili ya Familia.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anaialika Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza kuthamini kazi kama sehemu ya mchakato unaomshikirisha mwanadamu kazi ya kuumba na kuutawala ulimwengu; ni kielelezo cha kukuza uhuru wake; kwa kujitegemea na kuwategemeza wengine sanjari na kujenga umoja, ushirikiano na mshikamano na watu wengine ndani ya jamii. Waamini kwa namna ya pekee kabisa wanaalikwa kutathmini kazi kwa mwanga wa Injili.

Askofu mkuu Ruwa’ichi anawakumbusha waamini Jimbo kuu la Mwanza kwamba, wanapaswa pia kusherehekea maisha kwa: kusali, kuabudu na kushuruku, kujitathmini na kujipanga upya; kurekebisha na kusahihisha pale palipopinda. Mwaka wa familia iwe ni nafasi ya kusherehea zawadi ya maisha kwa kukumbuka matukio mbali mbali. Ni matumaini ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwamba, tafakari hii itaendelea kuwaimarisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika maisha, wito na dhamana ya Familia, ili kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya Familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.