2015-04-22 10:25:00

Katekesi kuhusu Familia: Dhambi imechafua mahusiano katika Ndoa!


Mwenyezi Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanaume na mwanamke. Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Baada ya kuhitimisha kazi ya uumbaji, Mwenyezi Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni ailime na kuitunza. Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano 22 Aprili 2015 mjini Vatican kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi kuhusu familia, maandalizi kwa ajili ya kuadhimisha Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke, ili waweze kukamilishana na kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mwanaume na mwanamke wameumbwa ili kuishi kwa pamoja, ili hatimaye, waweze kuingia katika agano la maisha. Dhambi ilipoingia katika maisha ya mwanadamu, ikaharibu mahusiano kati ya Bwana na Bibi; wakashindwa kuaminiana na hapo hali ya kudhaniana vibaya ikaingia katika maisha yao. Historia ya maisha ya binadamu inaonesha kwa namna ya pekee matokeo ya dhambi na kwa namna ya pekee dhidi ya wanawake, ambao wanadhulumiwa, wananyonywa na kutendewa ukatili.

Kutokana na dhana hii, katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na mwelekeo wa watu kutoaminiana na kudhaniana vibaya, hali ambayo imepelekea uwepo wa utamaduni wa baadhi ya watu kubeza maisha ya ndoa kati ya Bwana na Bibi; agano ambalo linaimarisha umoja, upendo na mshikamano na kulinda utu wao kama binadamu. Pale ambapo udumifu na matunda ya agano kati ya Bwana na Bibi yanabezwa na jamii husika; hapa ni mwanzo wa majanga kwa wengi, lakini waathirika wakubwa ni vijana. Licha ya dhambi na mapungufu ya kibinadamu; lakini wito wa binadamu ni kulinda na kutunza wito wa ndoa takatifu. Huu ni wito muhimu na wenye nguvu, unaomwezesha binadamu kushirikiana na Mwenyezi Mungu, ambaye analinda na kutunza matunda ya kazi yake ya uumbaji.

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa waamini na wahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, anawaombea ili Kristo mfufuka aweze kuwaimaarisha katika imani, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa upendo na huruma yake. Anawataka waamini kujenga na kuimarisha utamaduni wa kusali ili kweli familia ziweze kuwa ni shule ya sala. Familia zinazokabiliwa na magumu ya maisha, zitambue kwamba, ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu na msingi thabiti wa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, historia ya ukombozi inaonesha kwamba, pale ambapo mwanaume na mwanamke waliweza kuishi kwa kuzingatia amri na maagizo ya Mwenyezi Mungu, walibahatika kuishi kwa amani, furaha na utulivu, lakini pale waliporuhusu dhambi ichafue mahusiano yao, hapo wakaanza kukoseana heshima na kudhaniana vibaya. Waamini wamwombe Mwenyezi Mungu ili awasaidie kugundua ukuu wa agano kati ya mwanaume na mwanamke.

Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Siku ya 52 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa, Baba Mtakatifu anawataka: Wakleri na Watawa; Wanovisi na Majandokasisi kushuhudia kwa furaha wito ambao wameupokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watambue kwamba, dhamana na wito wa kimissionari si matunda ya nguvu zao binafsi, bali ni neema inayotoka kwa Mwenyezi Mungu; ambayo amewakabidhi mikononi mwao!

Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, tarehe 22 Aprili 2015, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Dunia, changamoto ya kuiangalia dunia kwa jicho la Mungu Muumbaji kwa kutambua kwamba, dunia na mazingira yake, yanapaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Mahusiano kati ya mwanadamu na mazingira yaoneshe uwiano bora; kwa kuyaheshimu, kuyatunza na kuyatumia kwa ajili ya huduma kwa binadamu na kwa vizazi vijavyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.