2015-04-21 10:43:00

Siku kuu ya Vesak: Wabudha na Wakristo pambaneni dhidi ya utumwa!


Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya Vesakh kwa ajili ya waamini wa dini ya Kibudha, inayoadhimishwa na nchi nyingi tarehe 3 Mei na kwa nchi nyingine, Siku kuu hii inaadhimishwa kati ya tarehe 25 Mei na tarehe 2 Juni kushikamana kwa dhati kupinga utumwa mamboleo. Siku kuu hii inakumbuka matukio makuu matatu katika maisha ya Gautama Budha: siku yake ya kuzaliwa, mwanga na kifo chake. Ni fursa ya kuwa karibu na watu wanaoteseka, ili kuwapatia faraja, amani na furaha kwa njia ya huduma inayojikita katika huruma.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya kuombea amani duniani kwa mwaka 2015, uliongozwa na kauli mbiu, “Si tena watumwa bali ndugu”. Utumwa mamboleo unajikita katika tabia ya kutowakubali wengine kuwa ni binadamu na matokeo yake ni kuwanyanyasa na kuwadhulumu: utu na heshima yao kama binadamu sanjari na kuwapokonya haki zao msingi; hali inayopelekea kukosekana kwa usawa kati ya watu. Mtumwa alinyimwa haki zake msingi na kuwa kama bidhaa. Ingawa biashara ya utumwa imepigwa rufuku duniani, lakini hata leo hii kuna mamillioni ya watu yanayoendelea kuishi katika hali ya utumwa kwa kunyimwa haki zao msingi.

Baba Mtakatifu anasema, hawa ni watoto wanaofanyishwa kazi za suluba; wahamiaji wanaonyanyaswa na kudhulumiwa utu na haki zao msingi kwa kulipwa ujira “kiduchu”; wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na ngono; kuna watu wanatekwa nyara kutokana na sababu mbali mbali; wengine wanauwawa kikatili. Yote haya ni matukio ya vitendo vya rushwa na kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna baadhi ya watu wanaoendelea kutajirisha kutokana na biashara haramu ya viungo vya binadamu. Haya ni madonda makubwa katika historia ya maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Budha anawakataza wafuasi wake kutojihusisha na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo na kwamba, watu wajipatie mahitaji yao msingi kwa njia halali na kwa amani bila kujihusisha na uvunjaji wa sheria. Kwa maneno mengine, dini ya Kibudha inataka watu kuheshimu maisha ya binadamu, uhuru na utu wake. Kumbe, Wakristo na Wabudha kwa pamoja wanaweza kusimama kidete kupambana na biashara ya utumwa mamboleo kwa kushinda ujinga, hali ya kutojali sanjari na kutoa huduma kwa waathirika wa utumwa mamboleo katika medani mbali mbali za maisha.

Ni matumaini ya Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini kwamba, maadhimisho ya Siku kuu ya Vesakh, yataweza kutoa faraja na furaha kwa watu wanaoteseka sanjari na kuendeleza ushirikiano kati ya Wakristo na Wabudha, ili kukomesha kabisa utumwa mamboleo. Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini umetiwa sahihi na Kardinali Jean Louis Tauran , Rais pamoja na Padre Migeule Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.