2015-04-21 08:19:00

Machafuko ya kijamii Afrika ya Kusini: ni kinyume cha ubinadamu!


Kardinali Wilfrid Napier, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban Afrika ya Kusini amewaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi mema barua ya kichungaji inayoonesha masikitiko yake makubwa kutokana na vurugu zilizojitokeza hivi karibuni nchini Afrika ya Kusini kwa misingi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Waafrika wanaoishi na kufanya kazi nchini Afrika ya Kusini. Kardinali Napier anawakumbusha wananchi wa Afrika ya Kusini kwamba hakuna sababu msingi inayoweza kuhalalisha vitendo vya kibaguzi dhidi ya binadamu wengine na kwamba, Afrika ya Kusini ni mali ya wananchi wote wanaoishi nchini humo, katika umoja unaojidhihirisha hata katika tofauti zao, wanajivunia kuwa Wabantu!

Kardinali Napier anasema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wa kichungaji, Kanisa katika ulimwengu mamboleo, maarufu kama Gaudium et spes, wanabainisha kwamba, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, hasa maskini na wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo la hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao. Kumbe, kuna haja ya kushirikiana na kushikamana na watu hawa badala ya kuwatesa na kuwanyanyasa.

Kardinali Napier anasema vurugu hizi ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu; mambo ambayo yanasigana na misimamo ya dini, changamoto na mwaliko wa kukataa kishawishi cha kufanya uhalifu kwa misingi ya ubaguzi wa rangi na woga usiokuwa na mashiko wala mguso. Jumuiya ya Kikristo haina budi kuwasaidia watu ambao wamelazimika kukimbilia kutoka katika maeneo yao na kuacha shughuli zao ili kusalimisha maisha yao. Jukumu hili linaweza kutekelezwa na mwamini mmoja mmoja, Parokia na Majimbo mbali mbali nchini Afrika ya Kusini.

Familia ya Mungu nchini Afrika ya Kusini inachangamotishwa kuhakikisha kwamba, maeneo yake yanakuwa ni mahali panapodhihirisha misingi ya haki, Amani, upendo na mshikamano wa kidugu. Tofauti baina ya watu zisiwe ni kisingizio cha uhalifu, nyanyaso na ubaguzi wa rangi, mambo ambayo yalizikwa wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini. Ikumbukwe kwamba, uhuru, Amani na utulivu wa Afrika ya Kusini kwa wakati huu ni mchango mkubwa uliotolewa na Nchi zilizoko Kusini mwa Afrika.

Ni ukarimu na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, mambo ambayo kamwe hayapaswi kusahauliwa na wananchi wa Afrika ya Kusini. Huu ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, muda wa kuwa kweli ni Wasamaria kwa watu wenye shida na mhangaiko mbali mbali. Wakristo wajitahidi kuwa ni wajenzi wa madaraja yanayowaunganisha watu katika misingi ya haki, Amani na mapendo ya kweli. Wawe ni vyombo na wajenzi wa Amani inayobubujika kutoka katika imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.