2015-04-21 09:02:00

Kilio cha damu ya Wakristo kinaendelea kusikika duniani!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya Wakristo 28 wa Kanisa la Kiethiopia waliokuwa wanaishi nchini Lybia. Haya ni mateso na machungu makubwa kwa Kanisa la Kiorthodox kuona watoto wake wakiuwawa kwa vile tu wanaungama imani kwa Yesu Kristo. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Patriaki Abuna Matthias wa Kanisa la Tewahedo la Kiorthodox nchini Ethiopia, anapenda kuonesha mshikamano wake na Kanisa zima na kwamba, yuko karibu nao kwa njia ya sala hasa wakati huu ambako kuna damu ya Wakristo wengi inaendelea kumwagika Barani Afrika, Mashariki ya kati na baadhi ya nchi Barani Asia.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni damu ya Wakristo inayoendelea kumwagika pasi na ubaguzi; ni damu ya watu wanaomkiri na kumshuhudia Yesu Kristo na kwamba, kilio hiki cha damu kinapaswa kusikilizwa na kila mtu ambaye anaweza kutofautisha kati ya wema na ubaya. Kilio cha damu kisikilizwe zaidi na watu wenye dhamana ya maisha ya raia wao.

Mama Kanisa anaendelea kumshangilia Kristo aliyefufuka kutoka kwa wafu, lakini furaha hii kwa mwaka huu imesheheni huzuni kubwa. Lakini Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, maisha ya Mkristo yako mikononi mwa huruma na upendo wa Mungu ambao ni mkubwa zaidi kuliko mateso na mahangaiko ambayo Wakristo wanaendelea kukabiliana nayo. Haya ni machungu ambayo wanashiriki watu wote wenye mapenzi mema kutoka dini mbali mbali. Kwa salam hizi za rambi rambi, Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Patriaki Abuna Matthias wa Kanisa la Tewahedo la Kiorthodox nchini Ethiopia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.