2015-04-21 07:29:00

Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo: Shule ya Neno, Sakramenti na Huduma


Mama Kanisa anapenda kuwekeza zaidi katika maisha na utume wa walei ndani ya Kanisa kwa kuwajengea uwezo ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kujisadaka kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zina mchango mkubwa sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Hizi ni shule za tafakari ya kina ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa njia ya matendo ya huruma. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC kwa kutambua umuhimu na dhamana ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 28 Oktoba 2015 litafanya mkutano kuhusu Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, huko Bangkok, Thailand.

Katika barua ya mwaliko iliyoandikwa na Askofu Patrick D’Rozario, Mwenyekiti wa Tume ya Walei na Familia, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia anabainisha kwamba, waamini walei wanahamasishwa na Mama Kanisa kuangalia kwa kina na mapana mahusiano yao na waamini wa dini nyingine kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika majadiliano ya kidini, changamoto makini iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita.

Waamini wanahamasishwa kumshuhudia Kristo na Kanisa lake kwa njia ya uhalisia wa maisha. Kumbe, majadiliano ya kidini ni kati ya changamoto kubwa kwa Kanisa Barani Asia, kama ilivyo pia kwa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano wa walei, utakuwa ni fursa ya kupembua: matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazoweza kutumiwa na waamini katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, ili kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano.

Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, wajumbe watabainisha mambo msingi yatakayokoleza mchakato wa ujenzi wa amani, udugu na mshikamano na waamini wa dini mbali mbali Barani Asia. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, mwezi Mei, litatoa mwongozo wa kufuata kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.